TAMBWE ARUDISHWA DAR

TAMBWE ARUDISHWA DAR

595
0
KUSHIRIKI
NA SAADA SALIM

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Amissi Tambwe, amerejeshwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mapumziko baada ya juzi saa nane usiku kuugua ghafla na kukimbizwa hospitali Visiwani Zanzibar alikokuwa na kikosi chake kinachoshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Tambwe amelithibitishia BINGWA kwamba amerejea jijini jana mchana kwa ajili ya mapumziko ya siku tano baada ya kugundulika kuugua malaria.

“Nimerudi nipo Dar es Salaam leo (jana) baada ya kuumwa ghafla na kupatiwa matibabu nikiwa Zanzibar katika majukumu ya timu yangu,” alisema Tambwe.

Wakati huo huo, Daktari wa Yanga, Edward Bavu, alisema Tambwe aliumwa ghafla juzi saa nane usiku na kupelekwa katika hospitali moja visiwani humo na kwamba hali yake inaendelea vizuri.

“Ana malaria, kwa hivyo atalazimika kukaa nje kwa siku tano, tumelazimika kumrejesha Dar es Salaam ili apatiwe matibabu zaidi,” alisema Dk. Bavu.

Tambwe atakosa mechi za hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kupewa mapumziko ya siku tano kwa ajili ya kurejesha nguvu baada ya kutumia dawa za malaria.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU