AZAM YAIFUATA URA FAINALI

AZAM YAIFUATA URA FAINALI

286
0
KUSHIRIKI

NA SAADA SALIM, ZANZIBAR

MABINGWA watetezi wa Kombe la Mapinduzi wametinga tena fainali ya michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo.

Azam wametinga fainali hiyo baada ya kuichapa Singida United bao 1-0 kwenye mchezo wa nusu fainali uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Amani Visiwani Zanzibar.

Mchezo huo ulikuwa wa aina yake na kuvutia kwa timu zote mbili kucheza kwa kushambuliana, ambapo dakika ya 11 mshambuliaji wa Azam FC, Enock Atta alikosa alipiga shuti lililopita pembeni ya lango la Singida United, kabla ya dakika moja baadaye nyota wa Singida, Malik Ntiri aliwekewa krosi nzuri na Kiggi Makasy lakini shuti lake lilitoka nje.

Mshambuliaji Bernard Arthur alijaribu kupiga shuti dakika ya 17 ambalo lilipaa nje na dakika ya 35 alipoteza nafasi ya wazi baada ya kumzidi nguvu beki wa Singida na kuugonga mpira uliotoka pembeni kidogo ya lango.

Timu hizo ziliendelea kushambulia kwa zamu, ambapo dakika ya 40, mshambuliaji Danny Lyanga alipiga shuti lililopaa juu ya lango la Azam na kipindi cha kwanza kumalizika bila ya kufungana.

Kipindi cha pili kilianza na Azam kufanya mabadiliko kwa kuwatoa Stephan Kingue na Atta na kuingia Frank Domayo na Iddi Kipagwile.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa Azam na kuonyesha dalili kwamba mchezo huo ungemalizika kwa sare kama ile nusu fainali ya kwanza, lakini dakika ya 78 nyota wa Azam, Shaban Idd ‘Chilunda’ aliifungia timu yake bao la ushindi akitumia vizuri mpira wa kurusha wa Bruce Kangwa.

Kwa ushindi huo Azam wamepata nafasi ya kutetea taji lao dhidi ya URA ya Uganda katika mchezo wa fainali utakaopigwa kesho Jumamosi.

Azam wakifanikiwa kunyakua taji hilo itakuwa wamelinyakua kwa mara nne, baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 2008 kisha 2012, 2013 na mwaka jana.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU