CHIRWA AITWA TENA KIKAANGONI

CHIRWA AITWA TENA KIKAANGONI

1395
0
KUSHIRIKI

NA MWANDISHI WETU

KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imempa nafasi ya mwisho ya kujitetea kwa mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa, baada ya kumsimamisha kwa muda usiojulikana.

Mshambuliaji huyo na kiungo wa Tanzania Prisons, Lambart Sabianka, walifungiwa na Kamati ya Mashindano ya TFF kwa kuzingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu kutokana na kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu.

Wachezaji hao wawili walifanya kosa hilo katika mchezo kati ya timu ya Yanga na Tanzania Prisons ambazo zilifungana sare ya bao 1-1 uliochezwa Novemba mwaka jana katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo, Boniface Wambura, alisema kamati ya nidhamu inatarajia kukaa tena Jumapili ijayo,  lakini kabla ya kutoa uamuzi wowote kwa Chirwa na  Sabianka watalazimika kusikiliza utetezi wao.

“Kamati ilikutana Jumapili iliyopita  lakini Chirwa na mwenzake hawakufika,  hivyo hakukuwa na maamuzi yoyote yaliyotolewa kwa kuwa tuliogopa kutoa uamuzi wa upande mmoja.

“Itakuwa nafasi pekee kwao kufika katika kikao cha Jumapili ambacho tutawasikiliza utetezi wao na kutoa hukumu kulingana na kanuni kwa kitendo walichokifanya,”  alisema Wambura.

Wakati huo huo, Wambura alisema wamefanya maboresho katika tuzo za kila mwezi, ambapo kwa Novemba mwaka jana ilinyakuliwa na kiungo wa Singida United, Mudathir Yahya.

Tuzo hiyo ambayo mshindi hupewa zawadi ya shilingi milioni moja kwa sasa ataongezewa ngao yenye jina lake pamoja na king’amuzi cha Azam TV.

“Fedha haitoshi kukumbuka alichokifanya kwa kuwa anaweza kuzipata na kuzitumia zote, hivyo tumeona bora kumzawadia ngao ambayo atakuwa akikumbuka kila akiiona.

“Ni zawadi ambazo zimeanza kutolewa kwa mshindi wa Novemba mwaka jana, baada ya kufuzu vigezo vya kuwa mchezaji bora,”   alisema Wambura.

Tuzo hiyo hupatikana baada ya maoni ya makocha na wachambuzi waliopo uwanjani kwa kufuata mwongozo wanaopatiwa na kamati ya tuzo ya TFF.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU