KICHUYA, MKUDE KIKAANGONI LEO

KICHUYA, MKUDE KIKAANGONI LEO

983
0
KUSHIRIKI

NA JAPHARY LESSO

KLABU ya Simba ya jijini Dar es Salaam leo inatarajia kutoa uamuzi juu ya wachezaji wao, Shiza Kichuya na Jonas Mkude, wanaodaiwa kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mapinduzi, Zanzibar dhidi ya URA ya Uganda, baada ya kukataa kukaa kwenye benchi walipofanyiwa mabadiliko.

Kitendo hicho kilionekana kuwakasirisha mno mashabiki na wanachama wengi wa Simba, wakitaka wachukuliwe hatua ili kukomesha tabia hiyo.

Kichuya alifanyiwa mabadiliko katika dakika ya 53 na nafasi yake kuchukuliwa na Mohammed Ibrahim `MO`, lakini alionekana kuwa mwenye hasira na kukataa kukaa katika benchi na badala yake kuelekea jukwaani kwa mashabiki kama ilivyokuwa kwa Mkude baadaye.

Akizungumza na BINGWA Dar es Salaam jana, Meneja wa Simba, Richard Robert, alisema kuwa mwafaka wa suala hilo utafanyika leo na uamuzi utakaoamuliwa, utatangazwa na Msemaji wa timu hiyo, Haji Manara, huku akisisitiza kuwa nidhamu lazima izingatiwe kwa kila mchezaji ili kutengeneza kikosi imara.

“Maamuzi yatatolewa mapema kesho (leo) na yatatangazwa na Msemaji wetu, Haji Manara. Kikubwa tunataka kudhibiti vitendo vya utovu wa nidhamu bila kujali ni nani amevifanya, kwani nidhamu ni muhimu sana katika klabu hivyo tunaomba uvumilivu,” alisema.

Kuhusu suala la wachezaji na viongozi wa timu hiyo kuzomewa na mashabiki walipotua jijini Dar es Salaam, Robert alisema halikuwa jambo la kiuungwana, lakini kilichosababisha hayo kutokea ni kutokana na  mashabiki hao kukerwa na kikosi chao kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Mapinduzi.

“Hakuna mtu anapenda kuzomewa na hatuwezi kufurahia hali hiyo, kwani tunajua si nzuri na imetuumiza sana, tunajua mashabiki wetu walikuwa wanahitaji matokeo ila hali imekuwa tofauti kwa sasa tutajipanga kurekebisha pale tulipokosea ili tuingie kwa kishindo Ligi Kuu,” alisema Robert.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU