TUKUTANE BANDARINI

TUKUTANE BANDARINI

586
0
KUSHIRIKI

SAADA SALIM, ZANZIBAR

SIKU chache baada ya Simba kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi na kuzomewa waliporejea jijini Dar es Salaam, sasa mashabiki wa timu hiyo wamewaambia mahasimu wao wa Yanga ‘tukutane bandarini’ ili nao walipe kiasasi.

Mashabiki hao wa Simba wanakisubiri kwa hamu kikosi cha watani wao wa jadi Yanga, baada ya jana kutolewa kwa penalti 5-4 kwenye mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya URA ya Uganda.

Kutokana na matokeo hayo, Yanga watarejea jijini Dar es Salaam kama watani wao wa jadi Simba, ambao walirudi juzi, baada ya kutolewa kwenye hatua ya makundi wakifungwa na URA bao 1-0 kwenye mchezo wao wa mwisho wa Kundi A.

Yanga wametolewa kwa mikwaju hiyo 5-4, baada ya dakika 90 za mchezo huo kumalizika bila ya kufungana ikiwa ni mara ya pili timu hizo kuamuliwa kwa matuta kwenye hatua hiyo ya nusu fainali na URA kushinda, ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2016.

Mchezo huo ulianza kwa URA kulishambulia lango la Yanga kwa takribani takika 15 huku wakipoteza nafasi kadhaa za mabao, kabla ya Yanga kufufuka na kufanya mahambulizi kadhaa, lakini dakika 45 za kwanza zilimalizika bila ya timu hizo kufungana.

Kipindi cha pili Yanga walionekana kujipanga upya, ambapo dkaika ya 52, Pius Buswita alishindwa kutumia pasi nzuri ya Papy Kabamba Tshishimbi na kupiga shuti lililookolewa na mlinda mlango wa URA, Alionzi Nafian kabla ya dakika ya 53 Obrey Chirwa kuingia kuchukua nafasi ya kiungo huyo wa zamani wa Mbao FC.

Lakini kuingia kwa Chirwa, ambaye alichelewa kujiunga na wenzake katika michuano hiyo alishindwa kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo.

Kocha wa URA, Ntala Paul naye alifanya mabadiliki dakika ya 69 akimwingiza Bokota Labama kuchukua nafasi ya Lwasa Peter, kisha Mulikyi Hudu alimpisha Ssempa Charles, ambaye alipiga shuti zuri dakika ya 77, lakini mlinda mlango wa Yanga, Youthe Rostand alionyesha umahiri wake kwa kuudaka mpira huo.

Nkomolwa na Ibrahim Ajib walipoteza nafasi za mabao dakika ya 75 na 77, kisha dakika chache baadaye wachezaji wa URA walimzonga mwamuzi wakitaka akubali kuwa bao mpira wa kichwa wa Lwassa uliopenya kwenye nyavu za pembeni na kuingia golini.

Kutokana na utovu huo wa nidhamu mwamuzi huyo alimpa kadi ya njano Kagaba Nicholas na hadi dakika ya 90 mchezo huo ulipomalizika hakuna nyavu zilizotingishika, hivyo ikabidi mshindi aamuliwe kwa matuta.

URA ndio walianza kupiga penalti ambapo wachezaji wao wote watano ambao ni Labama, Kibumba Enock, Kaenmu Shafik, Kulaba Jimmy, Briam Majwega na wote kutikisa nyavu za Yanga.

Penalti za Yanga zilizotinga kimiani ni zile zilizopigwa na Tshishimbi, Hassan Ramadhan Kessy, Gadiel Michael, Raphael Daud, ambaye aliingia dakika ya mwisho kwajili ya matuta na kupiga penalti na kali iliomvuruga kipa wa URA aliyeshindwa kujua aruke, kabla ya Chirwa kuwakera mashabiki wa Jangwani kwa kupiga penalti iliyoenda moja kwa moja mikononi mwa kipa.

Hii ni mara ya pili kwa URA kuingia fainali ya michuano hiyo, ambapo mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2016, ambapo waliifunga Mtibwa Sugar mabao 3-1 na kubeba taji hilo.

Kwa upande wa Yanga wameendelea kubaki na rekodi yao ya kutwaa taji hilo mara moja mwaka 2007, huku wakitolewa kwenye hatua hiyo ya nusu fainali kwa mara ya pili mfululizo baada ya mwaka jana kutolewa na watani zao Simba kwa matuta.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU