BATAMBUZE MIKONONI MWA LWANDAMINA

BATAMBUZE MIKONONI MWA LWANDAMINA

2194
0
KUSHIRIKI
NA SAADA SALIM, ZANZIBAR

YANGA wamejikuta wakinasa kwa beki wa kushoto wa Singida United, Shafiq Batambuze ambaye kiwango chake kimewavutia vigogo wa Wanajangwani hao na hivyo kulifikisha jina lake mikononi mwa Kocha Mkuu wao, George Lwandamina.

Batambuzi ameonyesha kiwango kizuri tangu amesajiliwa ndani ya kikosi cha Singida United kipindi cha usajili wa dirisha kubwa.

Taarifa za uhakika zilizoifikia BINGWA jana kutoka kwa kigogo mmoja wa Yanga, zinasema kwamba wameamua kulipeleka mapema jina la Batambuze kwa Lwandamina ili kuchukua nafasi ya Haji Mwinyi ambaye anatakiwa na AFC Leopards ya Kenya.

“Ni beki mzuri, nimefanikiwa kumuona katika mechi nyingi anazocheza yupo vizuri, pia ni muhimu kwetu sababu ya kuja kuchukua nafasi ya Haji aliyepata ofa Kenya,” alisema kigogo huyo ambaye hakutaka jina lake kuwekwa hadharani.

Kigogo huyo alisema AFC leopards bado wanamwinda beki wao, Mwinyi, hali inayowashawishi kutafuta mbadala wake mapema ambaye ni Batambuze.

BINGWA lilimtafuta Batambuze kufahamu kama ana taarifa juu ya mpango huo wa Yanga, ambapo alisema amesikia habari za kutakiwa na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini hadi sasa hajafuatwa rasmi, huku akikiri mkataba wake kubaki miezi minne, ukimruhusu kufanya mazungumzo na timu yoyote itakayomtaka.

“Kwa kuwa mkataba wangu sasa unaniruhusu kuzungumza na timu, Yanga waje tuzungumze,” alisema Batambuze, huku akigoma kuwe wazi dau lake.

Juu ya dili la Mwinyi kwenda AFC Leopards, BINGWA liliwasiliana na mwenyekiti wa klabu hiyo, Daniel Mule ambaye alisema mpango wao huo upo pale pale.

“Tunasubiri dirisha kubwa la usajili Juni mwaka huu tuanze mchakato wa kuingia mkataba na beki huyo wa Yanga,” alisema Mule.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU