BOCCO AKIPATA MPISHI SAHIHI, MTAMKOMA

BOCCO AKIPATA MPISHI SAHIHI, MTAMKOMA

1012
0
KUSHIRIKI
NA SAADA SALIM, ZANZIBAR

KOCHA wa URA ya Uganda, Paul Ntaka, amesema John Bocco ni miongoni mwa washambuliaji waliomvutia zaidi kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar, akidai kuwa nyota huyo wa Simba ni moto wa kuotea mbali.

Akizungumza na BINGWA jana, Ntaka alisema Bocco ni mshambuliaji mzuri mno, lakini amekosa watu sahihi wa kumtengenezea nafasi za kufunga mabao.

Alisema kwamba, katika timu zote tatu kutoka Tanzania Bara, yaani Simba, Azam na Yanga, hofu yake kubwa ilikuwa kwa mshambuliaji huyo, akiamini ndiye aliyekuwa tishio kwa kikosi chake kwenye michuano hiyo.

“Yule Bocco ni mzuri sana, anajua kufunga, nadhani Simba hawajapata mtu wa kumlisha mipira vizuri ili afunge, akipata mtu sahihi wa kumtengenezea mipira kwenye nafasi na muda sahihi, ni hatari sana,” alisema Ntaka.

Alisema japo hajawaona wachezaji wengine wa Simba ambao hawakushiriki michuano hiyo, lakini ana imani Wekundu wa Msimbazi hao wamekosa mtu wa kumfanya Bocco aweze kufunga kadiri atakavyo.

“Kama ningepata mtu kama Bocco katika kikosi changu, basi ningekuwa na uhakika wa kushinda idadi kubwa ya mabao katika kila mechi,” alisema.

Ntaka alisema pamoja na uwezo wake wa kufunga, Bocco ni msumbufu mno anapokuwa katika eneo la hatari la mpinzani wake.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU