MAPYA YAIBUKA MFUMO WA DJUMA

MAPYA YAIBUKA MFUMO WA DJUMA

1781
0
KUSHIRIKI
 NA SAADA SALIM, ZANZIBAR

WAKATI vuguvugu la mfumo mpya uliotumiwa na Kocha wa Simba, Masoud Djuma, kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi likiwa bado linaendelea, beki wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Abdi Banda, amesema mfumo huo si mpya Msimbazi kwani walishawahi kuutumia, lakini ukitegemea na ukali wa washambuliaji wa timu pinzani.

Akizungumza na BINGWA jana kutoka Afrika Kusini, Banda alisema wakati akiwa Simba, waliwahi kuutumia mfumo huo wa 3:5:2 enzi za kocha Dylan Kerry kwa mafanikio makubwa.

“Mfumo wa 3:5:2 tuliwahi kuutumia wakati tunafundishwa na Dylan Kerry, lakini unategemea na timu mnayokutana nayo. Unafaa mnapokutana na timu ambayo washambuliaji wake si hatari,” alisema.

Aliongeza: “Hatukuwahi kucheza mfumo huo wakati tunacheza na Azam FC au Yanga, kocha alikuwa akibadilisha kutokana na wapinzani wetu hao wanavyocheza, lakini pia kutegemea na aina ya wachezaji wetu waliopo kikosini.”

Alisema iwapo Djuma ataendelea kuutumia mfumo huo, ana imani Simba ikikutana na timu yenye njaa ya mabao, watafungwa mabao mengi.

Katika hatua nyingine, Banda amesema kitendo kilichofanywa na viongozi wa Simba kumuondoa aliyekuwa Kocha Mkuu wao, Joseph Omog, kitaigharimu timu yake hiyo ya zamani na kujikuta ikikosa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Alisema anaamini kilichomuondoa Omog Simba ni viongozi ambao hawaumizwi na timu hiyo na kuangalia masilahi yao binafsi, wakihitaji kupata asilimia fulani ya fedha kwa kuleta makocha wapya katikati ya msimu.

“Nacheza Afrika Kusini, huku wanamsifu (Joseph) Omog na (Hans van der) Pluijm, pia sioni sababu ya Simba kumuondoa kocha huyo (Omog), wangemwachia timu amalizie msimu… kwa mtindo huu, Simba wajiandae kumaliza ligi wakiwa nafasi ya tatu,” alisema.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU