SINGIDA UNITED YAIPIGIA SIMBA KAMBI DAR

SINGIDA UNITED YAIPIGIA SIMBA KAMBI DAR

808
0
KUSHIRIKI
NA SALMA MPELI

SINGIDA United imewasili Dar es Salaam na kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba, utakaochezwa Januari 18, mwaka huu, Uwanja wa Uhuru.

Kikosi cha Singida United kiliwasili jana kikitokea visiwani Zanzibar, ambako  kilikwenda kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi na baadaye kutolewa na Azam baada ya kufungwa bao 1-0, katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa juzi usiku  kwenye Uwanja wa Amaan.

Akizungumza na BINGWA jana, Mkurugenzi Mkuu wa Singida United, Festo Sanga, alisema baada ya kutolewa katika michuano ya Kombe la Mapinduzi sasa nguvu zao wanaelekeza Ligi Kuu Tanzania Bara.

Sanga alisema  kikosi chao kimeweka kambi katika Hoteli ya Rungwe, kikitarajia kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Uhuru.

“Timu inarejea leo (jana) saa nane mchana, tutaweka kambi Dar es Salaam  kujiandaa na mchezo wetu na Simba,” alisema Sanga.

Singida United wanashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo kutokana na pointi 23, huku Simba wakiongoza kwa pointi 26 sawa na Azam, lakini wakitofautiana mabao ya kufungwa.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU