DILI ZOTE ZA USAJILI ZILIZOFANYIWA UMAFIA CHINI YA MOURINHO

DILI ZOTE ZA USAJILI ZILIZOFANYIWA UMAFIA CHINI YA MOURINHO

911
0
KUSHIRIKI

LONDON, England

SI mara ya kwanza wala ya pili kwa timu anayofundisha Jose Mourinho kuwa kivuruge kwa timu nyingine, linapokuja suala la kusajili wachezaji nyota na tayari ametajwa kutaka kumchukua Alexis Sanchez mikononi mwa Pep Guardiola.

Ndiyo, Mourinho yuko kazini.

Kwa muda mrefu sasa nyota wa Arsenal, Sanchez, amehusishwa kuihama timu yake hiyo na kutua Man City kwa Guardiola.

Tetezi zilizoanza kuvuma mapema wiki hii zilisema kuwa Sanchez alikuwa kwenye hatua nzuri ya kumalizana na matajiri hao wa Manchester, lakini jioni ya juzi Jumatano, vyombo vikubwa vya habari nchini England viliripoti kwamba Mourinho na United yake walikuwa tayari kulipa fedha nzuri zaidi ya Man City ili kumchomoa nyota huyo Emirates.

Iwapo Mourinho atafanikiwa kumsajili Sanchez, utakuwa ni mwendelezo wa historia ya timu anayofundisha kupoka tonge mdomoni, iwe ni kwa mpango wake au wa timu.

Na hii ndiyo orodha ya mastaa wakubwa aliowahi kufanya umafia na kuwavutia kwake, asilimia kubwa ikiwa ni pindi alipokuwa akiinoa klabu ya Chelsea.

Willian kwenda Tottenham

Winga huyo wa Kibrazili alishakamilisha kila kitu kabla ya kutinga jezi ya Tottenham Agosti mwaka 2013 akitokea Anzhi Makhachkala, lakini Chelsea chini ya Mourinho ikaingilia kati na kumuiba nyota huyo.

Kitendo hicho kilisababisha uongozi mzima wa Spurs kukasirika mno.

Hasira za klabu hiyo zilishushwa kwa mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich, ambaye aliripotiwa kuwa kumbe aliwasiliana kwa njia ya simu na mmiliki wa Anzhi, Mrusi mwenzake, Suleyman Kerimov.

Tottenham wao walijua wazi kwamba tayari walishashinda vita ya kumwania Willian dhidi ya Liverpool na tayari winga huyo alishapimwa afya kwenye uwanja wa mazoezi wa Spurs, lakini mwisho wa siku alitua Chelsea.

John Obi Mikel kwenda Man Utd

Ishu ya Mikel ilianza hivi; jamaa alisaini nyaraka za kuondoka Lyn Oslo, Aprili mwaka 2005 na United ilifikia hatua ya kutangaza kwenye mtandao wao kwamba walishakamilisha dili la kumsajili kiungo huyo ambaye kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 18.

United ilifanya kosa kubwa la kuzungumza na mchezaji moja kwa moja bila uwepo wa wakala wake na licha ya mchezaji kuwakubalia kwamba angetua Januari mwaka 2006 na kumvisha jezi yao kwenye mkutano na waandishi wa habari, Mnigeria huyo hakwenda Old Trafford.

Mikel aliona kama vile alilazimishwa kusaini bila uwepo wa wakala wake na katika mahojiano rasmi, Mikel alifunguka wazi kuwa alitaka sana kujiunga na klabu ya Chelsea na si United.

Sekeseke hilo liliishia kwa Mikel kusaini mkataba wa kujiunga na Chelsea na baadaye klabu hiyo ililipa fidia kwa timu za Lyn na United.

Mo Salah kwenda Liverpool

Salah alinaswa na rada za klabu mbalimbali Ulaya kufuatia moto aliouwasha akiwa na FC Basel ya Uswisi, na kwa England ni Liverpool iliyoonesha dalili zote za kumsajili.

Mazungumzo yao na Basel yalikuwa yakiendelea, lakini yalichukua muda mrefu sana.

Mwisho wa siku Chelsea walitinga kwenye vita na bila ya kupoteza muda wakamsajili Salah huku aliyekuwa Mkurugenzi wa ufundi wa Liverpool, Ian Ayre, akinukuliwa akisema ‘kuna kupata na kukosa’, lakini wakala wa Salah, Sascha Empacher, alidai uzembe wa Liverpool uliwagharimu.

“Ujue ilichukua miezi miwili na nusu, mingi sana, timu zote zilikuwa nzito kukubaliana vitu kadhaa na Chelsea walipoivutia waya Basel, Salah akafurahia fursa. Haikuwa kwa sababu ya mambo ya kifedha.”

Florent Malouda kwenda Liverpool

Mwaka 2007, klabu ya Liverpool ilikutana na wizi wa mchana kufuatia winga huyo wa Kifaransa kubebwa na Chelsea kwa dau la pauni milioni 13 huku wao wakibaki wanang’aa sharubu.

Timu pekee ambayo Malouda alitabiriwa kuwa angetua ni Liverpool, wakati huo akiichezea Lyon.

“Rafa Benitez alinipigia simu mara kadhaa lakini hatukupata njia ya kunifanya nisaini kwao,” aliwahi kunukuliwa Malouda, ambaye ana rekodi ya kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Pedro Rodriguez kwenda Man Utd

Baada ya kuona maisha ya Barcelona yanazidi kuwa magumu kutokana na kwamba, miaka mitatu nyuma kulikuwa na utatu wa MSN; Neymar, Luis Suarez na Lionel Messi.

Manchester United ilimkaribia na kutaka kumnyakua, ila walikuwa wazito kukubali kumlipa mshahara alioutaka, ndipo ‘The Blues’ walipomvutia waya Pedro na kuzungumza naye.

Pedro alipokea simu kadhaa zikiwemo za Mourinho na Cesc Fabregas, ambaye aliwahi kucheza naye Nou Camp.

Mke wa Fabregas, Daniella Semaan, pia alimpigia simu mke wa Pedro, Carolina Martin na kumweleza kuhusu maisha yake ya London.

Kwa wakati huo, kigogo wa United, Ed Woodward alishajua mchezaji amekubali kutua Old Trafford.

Maskini! Kumbe Pedro alikuwa ameshapanda ndege ya London kuelekea Chelsea.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU