KWA TABIA HIZI UTAACHWA KILA SIKU

KWA TABIA HIZI UTAACHWA KILA SIKU

1461
0
KUSHIRIKI

ILI mahusiano yawe imara, kuna mambo ni lazima uyafanye na mengine ni lazima uyaache. Bahati mbaya watu wengi walio katika mahusiano hawajui ni mambo gani ya kufanya na mambo gani ya kuacha.

Baadhi wanaoamini wanajua mambo ya kufanya ili uhusiano wao uwe makini na imara, hufanya baadhi ya mambo ambayo kwao ni mazuri, ila yanaumiza mahusiano yao na kuyapa tafsiri tofauti.

Ni mara ngapi umeona wanaume wakiwapa wanawake mapesa mengi na kuwapeleka ‘outing’ za gharama kila siku, wakidhani hayo ndiyo mambo ya muhimu zaidi ya kujenga uhusiano wao?

Mahusiano ya kimapenzi hayajengwi katika namna za hovyo ama kukurupuka. Ili mahusiano yawe imara, kuna mambo ya msingi na makini zaidi yanatakiwa kufanywa kwa utulivu na weledi.

Baadhi ya wanawake wanadhani ili wapendwe sana inabidi wajiachie sana kingono kwa wahusika au inabidi wawe karibu na wapenzi kila muda.

Haya yanaweza kuwa sababu ya kupendwa. Ila hayawezi kuwa sababu halisi kama hayafanywi kimkakati na kwa mbinu mahususi.

Leo nataka tujadili sababu halisi za wapenzi wengi kupunguza mvuto wao kwa wahusika. Unajua sababu zenyewe? Ni hizi hapa.

KUWA MKOSOAJI SANA

KILA binadamu ana uzuri na ubaya wake. Na pia kila binadamu kiasili ni kiumbe mwenye kuhitaji kujaliwa, kusikilizwa na kuthaminiwa.

Kama mtu kwa sababu yoyote ile akawa ni mkosoaji sana kwa mhusika, akawa anajifanya anajua kila kitu, siyo tu atakuwa anamkera mhusika, ila pia mhusika atakuwa haoni fahari kukaa na yeye karibu.

Watu wanaojifanya wanajua sana na kuona wenzao hawajui kitu si watu ambao wanapendwa sana hata katika jamii. Kama wewe una tabia hiyo kwa mpenzi wako, yafaa ufahamu siyo tu unamkera, ila pia unamfanya asihitaji kuwa karibu na wewe.

KUPENDA KUONGELEA UNAYOPENDA

Asili ya kila binadamu ni mbinafsi (selfish). Ubinafsi huu unamfanya atawaliwe na hali ya kupenda yake yatekelezwe na yajadiliwe kila siku.

Sasa kama unataka mpenzi wako awe karibu na wewe, ajivunie kuwa na wewe, inabidi uoneshe hali ya kutaka kusikiliza na kujadili yake. Jisahau kwa muda.

Usipende sana kuongelea mambo yako. Yako yape muda mdogo ila yake yape muda mwingi. Mpe muda afurahie ubinafsi wake (ambao ni asili ya kila binadamu).

Mara nyingi penda kumsikiliza na kujadili mambo anayopenda yeye. Kwa kufanya hivyo, siyo tu atapenda kuwa karibu na wewe, ila pia atapata ithibati ya namna unavyompenda na kumjali.

Watu wengi hupenda kulazimisha mambo yao na vitu vyao tu ndivyo viwe mjadala pale wanapozungumza na wapenzi wao. Hali hii inakera na kuwaudhi wapenzi wao.

Hali hii inafanya wapenzi wao kujiona wana nafasi ndogo sana kwa wahusika. Wewe usiwe hivi kama unataka mwenzako akujali na akuthamini zaidi.

Ongelea vitu anavyopenda. Ongelea kila kitu kinachomfurahisha na kumburudisha. Kwa kufanya hivi unamfanya akuone wa thamani na maana kubwa katika maisha yake.

USIMBANE SANA

Huu ni mtihani kwa watu wengi. Wengi hudhani njia nzuri ya kumzuia mpenzi wake asimsaliti ni kumbana sana. Si kweli.

Ukimbana utamnyima uhuru wake wa kibinadamu wa kufurahi na kuona mengine. Hali hii itamfanya akuone kuwa kero kwake badala ya mpenzi wa kumpa raha na starehe.

Pia binadamu ni kiumbe mwenye kujawa na shauku ya kufanya jambo, hasa lile analoona anawekewa pingamizi.

Mfano, katika nyumba ya vyumba kumi, mtu anaweza kuishi hata mwaka mzima bila kuingia katika moja ya vyumba vya nyumba hiyo.

Ila siku ukimwambia rasmi kuwa asiingie katika chumba kile kile ambacho hajawahi kuingia, basi utaamsha ari ya kutaka kujua kunani katika chumba hicho.

Ndivyo iko hivyo pia ukimbana sana mpenzi wako. Ukijidai unachunguza sana simu yake, unamzuia sana kuongea na watu. Hali hiyo itamfanya afanye kweli.

Uhuru humfanya mtu aone mambo mengine ya kawaida na kukuangalia wewe katika uzito mwafaka. Ila ukimnyima uhuru huo utapata matokeo ambayo hata hutakaa uamini.

ramadhanimasenga@yahoo.com

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU