MAKOSA YA KILA SIKU HULETA VIRUSI VYA KUMALIZA PENZI

MAKOSA YA KILA SIKU HULETA VIRUSI VYA KUMALIZA PENZI

1932
0
KUSHIRIKI

MBALI na kuwa na msamaha ila kosa huacha aina fulani ya kumbukumbu kwa mhusika. Unaweza kukosea leo na ukapewa msamaha na mhusika akaahidi kusahau ila huwa kuna aina fulani ya kumbukumbu hubaki katika akili yake.

Makosa katika uhusiano huufanya uhusiano husika kuwa katika hali fulani ya kupooza. Ndiyo, binadamu hukosea na hakuna ambaye ataweza kuishi maisha pasi na kutenda kosa.

Pia kumewekwa msamaha kwa kila anayekosea. Ila kama makosa yenyewe ni ya kujirudia basi hufanya uhusiano husika kupoteza msisimko na maana.

Kwa anayekosewa kila siku huanza kuamini mwenzake hana hisia kamili na yeye ndiyo maana hufanya yale asiyopenda. Hawezi kukujali na kukuangalia katika mtazamo unaofaa ikiwa kila siku unamsababishia majuto na majonzi.

Mahusiano ni hali fulani ya kusababishiana raha, amani na utulivu wa nafsi. Ikiwa unamfanyia kinyume na haya inamaanisha unakaribisha aina fulani ya fikra kwa mwenzako.

Ni jukumu la kila mmoja kuwa makini katika uhusiano wake. Kuwa makini katika kauli na matendo yako. Mbali na kuwa na msamaha na kusamehewa, ila makosa ya kila siku yanafanya uhusiano ukose maana. Wengi wapo katika hali hii.

Baada ya kuwa na akina fulani na kuoneshwa kupendwa, walijisahau na kujikuta kila siku wanafanya makosa na matokeo yake leo, ile bashasha na raha ya uhusiano iliyokuwapo haipo tena.

Wengine leo wanalalama eti kwanini mahusiano yao hayana raha kama mwanzo wakiwa wamesahau ile raha imeondoka kutokana na wingi wa makosa yao kubadili namna ya kufikiria wenzao.

Mwangalie vizuri mpenzi wako. Mjali na kumthamini kwa kila jambo linalotakiwa. Mbali na hivyo, ila pia jiepushe na hali ya kumkosea. Yapo makosa ya kuepukika na si kila kosa huja bahati mbaya.

Kama kakwambia hataki aone unaongea na Amina kwanini unaongea naye? Kung’ang’ania kwako unajua unampa tafsiri gani. Kama unaona kuna ulazima wa kuongea na Amina ni suala la kukaa na mwenzako na kisha kuliongea kwa upana. Ukifanya tofaut ipo siku raha na amani iliyopo katika uhusiano wako itapotea kama shilingi katika jangwa na usiione.

Kuna kitu unatakiwa kufanya kwa manufaa ya mapenzi yako. Msikilize mwenzako na kisha msome na umuelewe. Leo unaweza kuona ni kawaida kukosea kwa sababu kila ukiomba msamaha anaelewa, ila unajua matokeo ya hali hiyo kwa baadaye?

Mfululizo wa makosa yako unaenda kutengeneza aina fulani ya fikra kwake. Fikra ambazo baadaye zitakuja kuyeyusha amani na furaha katika mahusiano yako.

Kila unapofanya kosa kuna maswali huwa anajiuliza. Hayo maswali baadaye ndiyo hutoa jibu litakalofanya akuone kama wewe si mtu mwafaka kwake.

Kinachotafutwa katika mapenzi si kuwa na mtu mwenye sura nzuri sana au kuwa na mtu mahiri sana kitandani pekee, hapana. Japo hayo ni mambo yana maana yake katika namna yake ila muhimu zaidi ni kuwa na mtu anayeweza kumsababishia furaha mwenzake.

Katika huzuni awe na uwezo wa kumfanya mhusika akatabasamu. Katika majonzi kuwe na hali ya unafuu na maisha kutoa maana chanya. Kama kila siku katika uhusiano ni makosa ya kujirudia ni kwa namna gani atakufikiria kama mtu mwafaka kwake?

Fikra zake ni lazima ziondoke katika kukufikiria kama mtu bora kwake na badala yake akuone mtu usiyefaa wala wa thamani katika maisha yake.

Japo huwa anasema anakusamehe ila kumbukumbu ya kosa lako huwa linabaki katika ubongo. Unaweza kufanya akaendelea kukuona bora kwa kufanya matendo bora na ya maana katika maisha yake.

Au unaweza kumfanya akakuona si lolote kwa kila siku kurudia yale ambayo unajua yanamsababishia simanzi na unyonge.

Nimeshawahi kusema kuwa, katika uhusiano hakuna kosa dogo. Kama  kitendo chako kinamtoa katika hali ya amani na furaha, hakijalishi kiko namna gani basi kichukulie kuwa ni kosa kubwa.

Msamaha huwa unafuta kosa katika meza ya majadiliano ila huwa hauondoi kumbukumbu nzima ya kosa. Kuwa makini na matendo yako. Suala si kusamehewa, ila ni kwanini kila siku unakosea wewe?  Kuwapo kwa msamaha si ruhusa ya kukoseana.

Mapenzi ni suala la hisia. Kama ukiweza kufanya kila siku akahisi amani na furaha ina maana atakuona mpenzi bora na kama utamfanya ajihisi mnyonge na kumpa mashaka, atakuona mpenzi usiyefaa. Kuwa makini.

Kama kweli unamhitaji katika maisha yako, mfanye awe na furaha. Epuka kumkosea na jitahidi kumfanya ajione kuwa kapata mtu sahihi na mwafaka katika maisha yake.

ramadhanimasenga@yahoo.com

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU