MR NICE: SIJUI WAZO LA KUANZISHA TAKEU LILITOKA WAPI

MR NICE: SIJUI WAZO LA KUANZISHA TAKEU LILITOKA WAPI

5457
0
KUSHIRIKI

Na CHRISTOPHER MSEKENA

HII ni Jiachie na Staa Wako, safu inayokupa uhuru wa kuuliza swali na kujibiwa na mastaa mbalimbali tunaokuwa nao hapa na kama nilivyokupa taarifa Jumanne iliyopita kuwa leo tutakuwa na nyota mkongwe wa muziki nchini, Lucas Mkenda ‘Mr Nice’, aliyetamba na mtindo wake wa Tanzania, Kenya na Uganda maarufu kama Takeu, karibu.

SWALI: Hamis Chagelo wa Vingunguti, Dar es Salaam anauliza ulilipwa shilingi ngapi kuonekana kwenye video ya Harmonize (Sina)?

Mr Nice: Tunaishi kwa kutegemeana, mtu kama anakufuata kwa uzuri huna sababu ya kukataa kwa sababu huwezi jua huko mbele mimi nitahitaji nini kutoka kwa wasanii kama yeye. Tuliongea kwa muda mrefu toka nipo nyumbani kwangu Nairobi mpaka anakwenda Marekani tunaongea.

WCB walimwambia Harmonize anifuate yeye mwenyewe halafu mengine wao watamsaidia, ndivyo ilivyokuwa ingawa siwezi kusema kama sikulipwa au nililipwa kiasi gani, binafsi mimi kufanya video na Harmonize nimefurahi ingawa yeye alifurahi zaidi.

SWALI: Danil Komba aliuliza ni kweli umefulia kama tunavyosikia?

Mr Nice: Watu lazima waseme hivyo kwa sababu wale niliokuwa nawanunulia kreti za bia nimeacha kufanya hivyo kwa hiyo watu kama hao lazima waone nimefulia, lakini sasa hivi nina majukumu, nina mambo mengi, nina watoto watatu na kila mmoja na mama yake na wanahitaji kwenda shule ila bata nakula kama kawaida.

SWALI: Tosh Lukombe wa Maranje Mtwara, anauliza unadhani kwanini wasanii wakifulia wanakimbilia kutumia dawa za kulevya?

Mr Nice: Siku zote nasema hao wanaotumia dawa wanafuata mstari wa kufa, acha wafe tu na Serikali iache kuwasaidia sababu hii nchi ina watoto yatima, jamii haina maji, hospitali na makazi.

Ukiingia huko kwenye dawa za kulevya unapotelea huko. Mimi ni mpambanaji ambaye ni adui wa dawa za kulevya na sijawahi kuvuta hata sigara, ila vimiminika vyeupe na ‘brown’ natumia sababu ni halali.

SWALI: Onesmo Faustine wa Ifakara anauliza mtindo wako wa Takeu ulianzisha vipi?

Mr Nice: Ni mawazo ambayo naweza kusema Mungu alinipa, unajua kila mtu ana kipawa chake kwa sababu ukiniuliza kwanini niliumiza kichwa na kupata Takeu ambayo mpaka leo hii ni kama nembo yangu siwezi kukujibu.

SWALI: Edward Lukowa wa Morogoro, anauliza kutokana na ukubwa wako hujawahi kusaidia wasanii chipukizi kama wanavyofanya mastaa wenzako.

Mr Nice: Siku zote mgonjwa ndiye huwa anafuata hospitali. Mimi siwezi kufanya kazi ya kutafuta wasanii ila wale wanaohitaji msaada wa Mr Nice wanakuja, waje tu ili tuone namna ya kusaidiana.

Kama kuna msanii anahisi naweza kumsaidia yeye ndiyo anitafute, mimi nina kampuni yangu inaitwa Takeu  Music Empire, hivyo mwenye uhitaji wa kitu fulani anitafute tunaweza kufanya.

SWALI: Abuu Mwinyimvua wa Morogoro, anauliza kitendo cha Young Dee kuurudia wimbo wako Kingasti umekipokeaje?

Mr Nice: Simjui Young Dee, sijawahi kukutana naye, mimi ninachojua kuna mwizi ameiba wimbo wangu, mambo mengi sipendi kuongelea kwenye vyombo vya habari ila ninachojua sheria zipo, muda utaongea.

SWALI: Geras Tweve toka pande za Makete, Njombe anauliza kwa sasa unamkubali msanii gani?

Mr Nice: Hakuna ninayemkubali kama Mr Nice, namkubali na ninamheshimu sana kwa sababu ni lazima upende nyumba yako ndiyo upende ya jirani.

SWALI: Juma Nyakunga wa Migoli Iringa, anauliza ni kweli wewe ndiye msanii wa kwanza Bongo kulipwa milioni 100 ya kufanya matamasha?

Mr Nice: Ilikuwa zaidi ya milioni 100 na ninalipwa fedha nyingi mpaka leo hii huko Rwanda, Kenya, Uganda, Malawi na kwingineko halafu nakuja Tanzania kutumia, hela ipo na mimi si mshamba wa hela kwa sababu nilianza kuwa nazo kabla ya muziki.

Mimi mchaga najua kutafuta hela, nafuga, nalima na ninaishi maisha ambayo wasanii wengi hawaishi.

SWALI: Mwizagu Said wa Kilwa anaulizwa ni kweli uliwekewa sumu kwenye chakula?

Mr Nice: Ni kweli, sijui aliyeweka alikuwa na lengo gani ila mimi nina tabia ya kusamehe na nahesabu kama ajali kwangu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU