DOZI YA SIMBA MORO USIPIME

DOZI YA SIMBA MORO USIPIME

5823
0
KUSHIRIKI

NA MWANDISHI WETU, MOROGORO


 

KAMBI ya Simba huko Morogoro imenoga si mchezo, huku Kocha Mkuu, Pierre Lechantre, akitoa dozi ya maana kuhakikisha wanashinda katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga.

Vinara hao wa Ligi Kuu wenye pointi 59, watavaana na watani zao, Yanga, keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Katika kujiandaa na mchezo huo, Simba jana ilifanya  mazoezi kwenye Uwanja wa Jamhuri, benchi la ufundi la timu hiyo, likiongozwa na Lechantre, lilikuwa na kazi moja tu ya kuwaelekeza wachezaji wa timu hiyo namna ya kupata mabao mengi.

Katika kuhakikisha mpango huo unatimia, Lechantre  alionekana kuwajenga wachezaji wake namna ya kumiliki mpira muda mrefu, kisha kuwapa mbinu viungo wake namna ya kupiga pasi za mwisho kwa washambuliaji wa timu hiyo, wakiongozwa na Mganda, Emanuel Okwi na John Bocco.

Baada ya kumaliza mazoezi mepesi ya kupasha moto misuli, Lechantre aliwagawa wachezaji wake katika makundi tofauti tofauti na kuanza kuwapa mbinu za kufunga mabao, ambapo aliwataka kupigiana pasi fupi na ndefu hadi kwenye eneo la sita kisha kufunga.

Mazoezi hayo yalikuwa ya nguvu mno, kwani Lechantre akisaidiana na wasaidizi wake, Masoud Djuma na kocha wa viungo, Mohammed Hbib, walikuwa wakali kutaka kila mchezaji afanye kwa ufasaha.

Kikubwa walichokifanya katika mazoezi hayo ni ujumbe tosha kwa wapinzani wao, Yanga, waliozoea kuwaita wamatopeni au mchangani.

Katika kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo huo, Kocha Msaidizi Djuma alisema lengo la mazoezi hayo ni kuwaweka fiti na kuwafanya wachezaji wawe na nguvu na wepesi tayari kucheza na timu yoyote.

“Programu ya leo (jana) ni mbio kama tulivyofanya asubuhi na jioni, lengo ni kuhakikisha wanakuwa na nguvu za kutosha katika kujiweka sawa na mchezo huo.

“Tunawaheshimu wapinzani wetu, ni timu kubwa kama sisi, ina wachezaji wazuri, mchezo hautakuwa rahisi, kila mmoja anataka ushindi, tunaendelea kujipanga kwa mbinu, kisaikolojia kuhakikisha tunaibuka na ushindi.

Djuma alisema kuwa, wanahitaji pointi tatu katika mchezo huo, ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa huo, unaoshikiliwa na mahasimu wao wa jadi kwa miaka mitatu mfululizo.

Simba, iliyoweka kambi Morogoro kujiandaa na mchezo huo, ina pointi 59, baada ya kucheza michezo 25, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 48 katika mechi 23 ilizocheza.

Simba na Yanga zitakutana Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya awali kutoka sare ya bao 1-1.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU