YONDANI KIMEELEWEKA YANGA SC

YONDANI KIMEELEWEKA YANGA SC

3822
0
KUSHIRIKI

NA HUSSEIN OMAR


 

*Ni baada ya kikao kizito Jangwani jana, apaa na timu kukinukisha Sportpesa Kenya

*Cannavaro ajitia pingu mwaka mmoja Yanga

BEKI kisiki wa Yanga, Kelvin Yondani, hatimaye amemalizana na uongozi wa klabu yake hiyo baada ya kuzungumza nao jana katika makao makuu ya Wanajangwani hao na kukubaliana nao kuongeza mkataba mpya.

Baada ya hapo, Yondani aliungana na wenzake waliotarajiwa kuondoka jana jioni kwenda Kenya kushiriki michuano ya Sportpesa Super Cup itakayoanza wikiendi hii mjini Nakuru.

Hatua ya Yanga kufanya mazungumzo na Yondani jana, imekuja baada ya tetesi kuwa nyota huyo alikuwa akifukuziwa na Simba, Azam FC na Singida United, lakini pia msimamo wake wa kutaka mkataba mpya kwa kuwa wa awali umemalizika.

Yondani amekuwa na kiwango bora ndani ya Yanga tangu alipojiunga nayo msimu wa 2013/14 akitokea Simba, lakini aking’ara zaidi msimu huu wakati timu yake hiyo ikikabiliwa na lundo la majeruhi, lakini pia ukata uliowafanya baadhi ya wachezaji kutojituma tofauti na ilivyokuwa kwa beki huyo ambaye alikipigania kikosi chao kwa nguvu na uwezo wake wote.

Akizungumza na BINGWA jana, Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten, alisema mazungumzo baina ya Yondani na uongozi yamekwenda vizuri na muda wowote kuanzia sasa, atasaini mkataba mpya kuichezea timu hiyo msimu ujao.

“Mambo yamekwenda vizuri. Yondani alikuwa na mazungumzo ya muda mrefu na viongozi kuhusu mkataba mpya na amekubali kuongeza mkataba mpya baada ya majadiliano hayo,” alisema Ten.

Ten alisema Yondani pia amekubali kusafiri na timu kwenda Kenya kushiriki michuano ya Sportpesa itakayoshirikisha timu kutoka Tanzania na nchini humo.

Itakumbukwa nyota huyo aliwahi kuliambia gazeti hili kuwa hataki kuishi maisha ya kutia huruma atakapostaafu soka na ndio maana amewakomalia matajiri wake kuweka fedha mezani ili asaini mkataba mpya.

Alisema hataki kusikia siasa katika suala zima la kuongeza mkataba mpya wa kuichezea timu hiyo kwani iwapo atafanya kosa hilo, linaweza kumgharimu maisha yake yote.

Beki huyo alitoa kauli hiyo baada ya kugoma kuongozana na timu yake ilipokwenda nchini Algeria kuvaana na USM Alger ya huko, katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Sitaki kudhalilika, umri unakwenda, muda wangu wa kucheza mpira uliobaki ni mchache, hivyo sitaki kufanya makosa kama wengine, nataka heshima, waweke fedha nisaini,” alisema Yondani.

“Japo ninaipenda sana Yanga, nikiwa nimeitumikia kwa nguvu na moyo wangu wote, tena kipindi wale wanaothaminiwa wakiwa hawatoi mchango wowote kwa kisingizio cha majeraha. Haya ni maisha, nipo Yanga kikazi, sitaki baadaye nije kuchekwa,” alisisitiza.

Akimzungumzia mchezaji huyo, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, amesema wamejipanga kuhakikisha wanampa mkataba mnono ambao utamfanya aendelee kufurahia maisha yake katika klabu hiyo ya Jangwani.

“Wataondoka wote lakini si Yondani, ni mtu muhimu sana kwetu. Tumejiridhisha kwa kila hali kuwa Yondani ana mapenzi makubwa na timu, lakini pia amekuwa ni mmoja wa wahamasishaji wazuri kwa wenzake uwanjani,” alisema Mkwasa.

Katika hatua nyingine, nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kuitumikia timu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Cannavaro alikuwa ni miongoni mwa wachezaji waliomaliza mkataba na mabingwa hao wa zamani wa Bara ambao msimu huu wameambulia nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC, iliyoshika nafasi ya pili, huku Simba wakitwaa ubingwa.

Akizungumza na BINGWA juzi katika makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Mtaa wa Jangwani, Dar es Salaam, mkongwe huyo alithibitisha kusaini mkataba huo, huku akipanga kurejea darasani kusomea ukocha.

“Nataka nimalize mpira wangu nikiwa Yanga, pia nataka nicheze huku nikiwa nasomea ukocha na masomo mengine kwa ajili ya kuandaa maisha yangu ya baadaye,” alisema Cannavaro.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU