DILUNGA: NIPO TAYARI KUTUA YANGA TENA

DILUNGA: NIPO TAYARI KUTUA YANGA TENA

2888
0
KUSHIRIKI

NA HUSSEIN OMAR


KIUNGO mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Hassan Dilunga, amesema yuko tayari kumwaga wino Yanga kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Dilunga, ambaye kwa sasa amekuwa moto katika kikosi cha Mtibwa Sugar na kuisaidia timu yake hiyo kutwaa Kombe la Azam, awali aliweka wazi hana mpango wa kurejea Jangwani, kabla ya kubadili maamuzi yake hayo hivi karibuni.

Nyota huyo amekuwa akihusishwa kurejea Yanga kwa muda mrefu, tangu msimu uliopita na kipindi cha dirisha dogo msimu huu.

Dilunga alijiunga na Mtibwa Sugar akitokea JKT Ruvu, ambayo kwa sasa inaitwa JKT Tanzania, aliondoka Yanga kutokana na kukosa nafasi kikosi cha kwanza.

Tangu ajiunge na Mtibwa, kiwango chake kimeimarika kiasi cha kupata namba ya kudumu katika kikosi cha kocha Zubery Katwila, jambo linalosababisha wadau wa soka kuanza kuhisi msimu ujao anaweza kuonekana katika kikosi chake cha zamani.

Akizungumza na BINGWA jana, Dilunga alisema anajisikia furaha kuwapo Mtibwa Sugar, lakini kama Yanga wataweka mzigo wa kutosha mezani, yupo tayari kufanya kazi na Wanajangwani hao.

“Zipo timu nilizopitia kabla ya kujiunga na Mtibwa Sugar, ikiwemo Yanga na JKT Tanzania na wameonyesha nia ya kutaka nirudi, sina tatizo, waweke mzigo wa kutosha tufanye kazi,

“Mimi ndiye najua maisha gani nilipitia kule nilikotoka na ninayoishi sasa hivi hapa Manungu, nimejifunza mengi na nimekua kiakili kwa sasa hivi siwezi kufanya tena makosa, nataka nifanye kazi,” alisema.

Dilunga, ambaye aliachwa na Yanga katika kipindi cha dirisha dogo la ligi hiyo, lililofungwa Desemba 15 msimu wa mwaka 2015/16, alisema watakuwa tayari kuichezea Yanga iwapo watatimiza masharti yake, mchezaji huyo amefunga mabao sita msimu huu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU