BADO MAKOSA MLIYOWAHI KUKOSEANA YANATESA MAHUSIANO YENU? FANYA HIVI

BADO MAKOSA MLIYOWAHI KUKOSEANA YANATESA MAHUSIANO YENU? FANYA HIVI

1301
0
KUSHIRIKI
Relationship difficulties

KUNA watu walikoseana toka mwezi wa kwanza ila hadi sasa bado hisia zile za ugomvi zinawatesa katika maisha yao. Hawana amani wala raha kutokana na makosa yale.

Kila uchao katika maisha yao badala kuwe na taswira mpya ya furaha na amani, ila bado ule mzimu wa makosa uliowahi kutokea unawaandama. Upo katika kundi hili?

Itambulike ili kumaliza ugomvi uliowahi kuwatokea, inabidi kusiwepo tena mjadala unaouhusu. Hisia za ugomvi ama mvurugano hutawala ikiwa bado kuna mijadala ama ukumbusho kuhusiana na hali hiyo.

Ili amani na furaha ipatikane kwa wapenzi waliowahi kukosana inabidi kusiwepo tena na mjadala ama kukumbushia kilichowahi kutokea.

Kitendo cha kukumbushia ulivyowahi kukosewa na mwenzako hakuleti utulivu baina yenu ila unachochea mitafaruku zaidi.

Binadamu ni kiumbe asiyekubali kushindwa.

Kama wewe unapenda kukumbushia juu ya makosa aliyowahi kukufanyia, haitoshangaza na yeye kukumbushia baadhi ya madhila yako.

Hali ikiwa hivyo amani baina yenu itatoka wapi?

Njia sahihi ya kuzika hisia za makosa yaliowahi kutokea baina yenu ni kuacha mara moja kuzungumzia namna alivyowahi kukusokea.

Ili mtu afurahie mahusiano yake kwa kiwango kikubwa inabidi awe na amani juu ya hisia na fikra zake. Na njia sahihi ya kuwa na amani katika hisia na fikra zake, ni ile hali ya kujiona hana hatia katika maisha yake.

Sasa mwenzako atafurahia vipi mahusiano yenu ikiwa unamfanya ajione mkosefu kwa kukumbushia makosa aliyowahi kukufanyia?

Katika mahusiano kuna changamoto nyingi. Ila watu makini wenye kuweza kuishi kisahihi ndio huweza kupunguza ukubwa wa changamoto hizo na kujikuta wakiwa na furaha katika mahusiano yao.

Amani katika nyumba yako itatawala ikiwa kuna hisia na kumbukumbu ya mambo ya furaha na yenye kutia msisimko. Mfanye mwenzako afurahie uwepo wako na akumbuke nyakati njema zingine amabazo mmewahi kuishi kwa pamoja.

Hisia za mapitio mema zitamfanya mwenzako azidi kusisimkwa na wewe. Ila kama kila leo unamfanya ajione mkosefu anaweza kujikuta akiwaza namna ya kukuepuka.

Watu wanaingia katika mahusaiano, pamoja na mambo mengine ni kupata afueni ya shida za kidunia. Binadamu ni kiumbe mwenye kupenda raha na amani.

Uamuzi wake wa kuingia katika mahusiano na wewe shabaha yake ilikuwa ni kupata raha na amani. Sasa acha kumtesa kwa kumfanya ajihisi mkosefu.

Japo binadamu ni dhaifu ila hapendi kuonwa mkosefu kila mara. Kupima hali hiyo angalia watu wasivyopenda kukosolewa. Japo kila siku tunaimba kwamba hakuna binadamu aliyekamilika, ila ukweli uliowazi ni kwamba mtu huwa hajihisi amani sana kama akikosolewa.

Ukweli huu ukufanye kujua kuwa unatakiwa kujifunza kupotezea mapema makosa mnayosameheana ili maisha yenu yazidi kujawa na nuru ya amani na furaha.

Mwenzako anapokukosea hakikisha unapambana na tatizo husika na sio kukumbushia lundo la makosa aliyowahi kukufanyia.

Kukumbushia alivyowahi kukukosea hakusababishi utulivu baina yenu ila utachochea na yeye aanze kutaja idadi na aina ya makosa uliyowahi kumfanyia.

Maisha yatakupa raha ikiwa utajifunza kuwa makosa yapo na njia rahisi ya kupambana nayo ni kutoyapa mazingatio katika fikra zako. Kuishi na kinyongo cha makosa aliyowahi kukufanyia sio tu unajiumiza mwenyewe ila pia unafanya mahusiano yako yasitawaliwe na amani.

Usidhni ni wewe tu unayekosewa. Wengine wanakosewa zaidi ya unavyokosewa ila unaona amani katika mahusiano yao kwa sababu wanajua njia nzuri ya kupambana na makosa yao.

Hakikisha baada kumaliza ugomvi wako na mwenzako hurudii tena kuzungumzia hilo kosa. Kupenda kuzungumzia kosa ni mbolea inayootesha tatizo lililo taabani.

ramadhanimasenga@yahoo.com

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU