BADO WAO

BADO WAO

7149
0
KUSHIRIKI

SAADA SALIM, DAR NA TIMA SIKILO, PWANI

MABAO ya nahodha John Bocco, Emmanuel Okwi na Asante Kwasi katika kipindi cha kwanza yalitosha kuhakikishia Simba inaendelea kujichimbia kileleni mwa Ligi Kuu Bara.

Swali linabaki, nani wa kuizuia Simba msimu huu? Ikicheza kwa kujiamini katika kipindi cha kwanza, Simba iliifunga Mbeya City mabao 3-1 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Baada ya matokeo hayo, Simba ambao wamecheza michezo 23 wamefikisha alama 55 ikiwa ni pointi nane zaidi ya mpinzani wao wa karibu Yanga ambao pia ni mabingwa watetezi lakini wanao mchezo moja mkononi.

Iliwachukua dakika 16 kwa Simba kupata bao la kuongoza lililofungwa kiufundi na mshambuliaji raia wa Uganda, Okwi, kwa guu lake la kushoto kutokana na mpira uliotemwa na kipa wa Mbeya City, Owen Chaima akipangua shuti lililopigwa na Bocco.

Simba walizidisha mashambulizi zaidi na dakika ya 32 Kwasi aliiandikia timu hiyo bao la pili kwa kichwa kutokana na mpira fupi wa kona uliyopigwa na Kichuya ambaye alianzishiana na Shomari Kapombe.

Bao hilo lilidumu kwa dakika moja tu kabla Frank Ikobela wa Mbeya City kuifungia timu yake bao la kufuta machozi dakika ya 33 kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona iliyopigwa na Danny Joram.

Furaha hiyo ya Mbeya City ilikatishwa dakika moja baadaye baada ya Simba kufanya shambulizi kali na la kushutukiza lililowahusisha Okwi na Kapombe na mpira kumkuta Bocco aliyefunga bao la tatu.

Hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa mabao 3-1, huku Wekundu hao wa Msimbazi wakionekana kuutawala zaidi mchezo huo kwenye kipindi hicho cha kwanza.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Mbeya City wakionekana kubadilika kimchezo na kufunguka zaidi tofauti na awali na kubadilishana mashambulizi na wapinzani wao Simba.

Dakika 53 nusura Okwi aipatie Simba bao la nne kwa shuti kali akipokea pasi ya Bocco, lakini mpira uligonga mwamba wa juu na kutoka nje na dakika tano baadaye, Kichuya alipiga shuti lakini umakini wa kipa wa Mbeya City, Owen Chaima, aliokoa hatari hiyo.

Ikobela alijibu mashambilizi dakika ya 65 kwa shuti akipokea pasi ya krosi ya Victor Hangaya na dakika 85, Haruna Shamte, alijaribu kutaka kuipatia timu yake bao kwa mpira wa faulo lakini shuti lake lilikwenda nje.

Hadi firimbi ya mwisho ya mwamuzi wa mchezo huo, Hannce Mabena kutoka Tanga, matokeo yalibaki 3-1, Simba wakijikusanyia pointi zote tatu muhimu na kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Bara uliochezwa jana Uwanja wa Manungu mjini Turiani, Morogoro, wenyeji Mtibwa Sugar waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda FC kutoka Mtwara.

Bao hilo la pekee lilifungwa na mshambuliaji Kelvin Sabato ‘Kiduku’ dakika ya 22.

Mchezo wa ligi kati ya Ruvu Shooting dhidi ya Azam FC uliotarajiwa kuchezwa jana ulihairishwa na utachezwa leo katika Uwanja wa Mabatini, mkoani Pwani.

Kamisa wa mchezo huo, Peter Temu, akishirikiana na waamuzi walifikia maamuzi ya kuhairishwa mchezo huo kufuatia mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha uwanja kujaa maji.

Akizungumza na BINGWA jana, Temu alisema wangeweza kuruhusu mchezo uendelee lakini sheria hairuhusu kwasababu baada ya kukagua uwanja wamejiridhisha ulikuwa umejaa maji na usingiwezekana kutumika ukiwa katika hali hiyo.

“Kama ambavyo mmeona wachezaji walijiandaa vizuri lakini kutokana na ukubwa wa mvua itabidi uchezwe kesho (leo) saa kumi jioni,” alisema

Azam wanashika nafasi tatu kwenye msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi 23 na kuvuna pointi 45.

Kikosi cha Simba; Aishi Manula, Nicholas Gyan/James Kotei dk87, Asante Kwasi/Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ dk72, Juuko Murshid, Yusuph Mlipili, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Emmanuel Okwi, John Bocco/Laudit Mavugo dk79 na Shiza Kichuya.

Kikosi cha Mbeya City; Owen Chaima, Rajabu Isihaka, Majaliwa Shabani, Ally Lundenga, Haruna Shamte, Eliud Ambokile, Danny Joram/Mohamed Samatta dk61, Victor Hangaya/Geofrey Muller dk79, Babuu Ally/Hamidu Mohamed dk44 na Frank ikobela.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU