DAKIKA 7 ZILIVYOWANYIMA TP MAZEMBE MIL 200 ZA SUPER CUP

DAKIKA 7 ZILIVYOWANYIMA TP MAZEMBE MIL 200 ZA SUPER CUP

818
0
KUSHIRIKI

PRETORIA, Afrika Kusini

MWISHONI mwa wiki iliyopita, mashabiki wa soka walipata burudani ya kutosha kwa kushuhudia mchezo mkali wa michuano ya Super Cup kati ya Mamelodi Sundowns na TP Mazembe.

Mazembe waliingia kwenye mchezo huo wakiwa mabingwa watetezi, kwani ndio waliochukua taji hilo mwaka jana.

Lakini, hawakuwa na kibarua chepesi kulitetea taji lao hilo, kwani walikuwa wakivaana na mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pia, Mazembe waliingia uwanjani wakiwa kifua mbele, hasa kutokana na rekodi yao ya kuchua taji la Ligi ya Mabingwa mara tano, huku wapinzani wao hao wakiwa wamebahatika mara moja tu.

Mtanange huo ulipigwa kwenye Uwanja wa Lucas Masterpieces Moripe, uliopo mjini Pretoria, Afrika Kusini, na wenyeji Mamelodi Sundown wanaonolewa na kocha Pitso Mosimane waliibuka kidedea.

Bao pekee la Mamelodi liliwekwa kimiani na beki wa kati, Ricardo Nascimento, ambaye alifunga zikiwa zimebaki dakika saba kabla ya kumalizika kwa mchezo huo.

Ni kama ilikuwa siku ya Nascimento, kwani dakika ya sita ya mchezo huo alikosa bao la wazi baada ya mpira aliopigwa kwa kichwa kutoka nje kidogo ya lango la Mazembe.

Kwa wasiofuatilia Ligi Kuu Afrika Kusini (PSL), nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 ni raia wa Brazil na anacheza nafasi ya ulinzi. Aliwahi kupita katika klabu ya Palmeiras, lakini hakubahatika kupata nafasi kikosini.

Mamelodi, ambao ndio mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, waliuanza mchezo huo kwa kasi na almanusura wapate bao katika sekunde ya 18.

Wakali hao wa soka la ‘Sauzi’ walikosa bao la wazi baada ya nyota wao, Themba Zwane, kushindwa kukwamisha mpira wavuni akiwa na mlinda mlango wa Mazembe, Ghead Grisha.

Kwa ushindi huo, Mamelodi wamejinyakulia kitita cha Dola za Marekani 100,000 (sawa na zaidi ya Sh milioni 200 za Tanzania).

Kwa upande wao, Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeondoka na Dola 75,000.

Lakini pia, hilo ni taji la kwanza kwa Mamelodi, licha ya kucheza michuano ya Super Cup mara 25.

Aliyesababisha majanga kwa Mazembe ni beki wake, Issama Mpeko, ambaye alimchezea madhambi nahodha wa Mmelodi, Homphela Kekana, katika eneo la hatari.

Kwa matokeo hayo, Mamelodi wameweka historia ya kuwa timu ya pili kutoka Afrika Kusini kuchukua taji la Super Cup.

Timu ya kwanza kufanya hivyo ilikuwa Orlando Pirates, ambayo ilicheza mwaka 1996 na kuibuka na ushindi mbele ya JS Kabylie ya Algeria.

Mbali na rekodi hiyo, Mamelodi ni timu ya pili kutoka Afrika Kusini na kunyakua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hiyo ilikuwa mwaka jana, baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 3-1 katika michezo miwili ya fainali dhidi ya mabingwa wa soka nchini Misri, Zamalek.

Ikiwa hii ni mara ya kwanza kwa Mamelodi kushinda taji hilo la Super Cup, wenzao, Mazembe wamelifungia kabatini mara tatu (2010, 2011 na 2016).

Vikosi vilikuwa hivi:

Mamelodi Sundowns: Onyango, Morena, Arendse, Nascimento, Langerman, Mabunda, Kekana, T Zwane/Vilakazi, Laffor/Soumahoro, Billiat/Ngcongca, Tau

TP Mazembe: Gbohouo, Issama, Kimwaki, Coulibaly, Kasusula, Sinkala, Adjei, Kalaba/A Traore, Asante, Malango, Elia/Mputu

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU