DJUMA HUYOO YANGA

DJUMA HUYOO YANGA

3380
0
KUSHIRIKI

AYOUB HINJO NA SAADA SALIM

KOCHA msaidizi wa Simba, Mrundi Masoud Djuma, ni miongoni mwa majina yaliyopendekezwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji wa Yaga kuchukua nafasi ya George Lwandamina aliyejiunga na timu yake ya zamani ya Zesco United ya Zambia.

Kamati hiyo ya Yanga ilikutaa juzi usiku jijini Dar es Salaam baada ya mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida United, uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Yanga, zilizoifikia BINGWA jana, zinasema kwamba Djuma ametajwa sana katika kikao hicho kilichofanyika takribani kwa saa tatu katika makao makuu ya timu hiyo.

Chanzo chetu cha uhakika ambaye hakutaka jina lake kuwekwa hadharani, alisema kwamba baada ya kuondoka kwa Lwandamina, uongozi wao upo katika mchakato wa kumtafuta kocha atakayerithi nafasi ya Mzambia huyo.

“Tulikuwa na majina mengi, lakini Djuma amekuwa akitajwa sana katika kikao hicho, pia kabla ya hapo, alishawahi kuzungumziwa kuchukua nafasi ya Lwandamina,” alisema mtoa habari huyo.

Alisema kabla ya taarifa za kuondoka kwa Lwandamina juzi, awali walipata tetesi hizo, hivyo uongozi wa Yanga ulianza kumfuatilia kwa ukaribu Djuma, hasa baada ya Simba kuwa katika mchakato wa kumsaka kocha mkuu pale Mcameroon Joseph Omog alipotimuliwa.

Chanzo hicho kilisisitiza kuwa wana uwezekano mkubwa wa kumnasa Djuma ambaye hawana shaka naye katika ufundishaji, hasa kwa wakati huu ambao mkataba wake na Simba haujawekwa wazi.

“Tunafahamu kuwa Djuma aliondoka Rayon Sports (ya Rwanda) ili aje kuwa Kocha Mkuu wa Simba, lakini mambo yamebadilika. Hadi sasa mkataba wake haufahamiki, tunaamini lazima tutampata,” alisisitiza.

BINGWA lilipomtafuta DJuma kuzungumzia suala hilo la kutakiwa na Yanga, alionekana kupata kigugumizi kabla ya kukana kufuatwa na kiongozi yoyote wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuhitaji huduma yake ndani ya klabu hiyo.

“Hizo habari kwangu mpya, nadhani ni maneno ya kijiweni,” alisema Djuma kwa kifupi mna kuhamia katika mada nyingine katika kile kilichoonekana kuepuka kuchimbwa zaidi juu ya suala hilo.

Ukiachana na Djuma, makocha wengine wanaopewa nafasi ya kurithi mikoba ya Lwandamina Yanga ni kocha wa Mbao FC, Etienne Ndayiragije ambaye hata hivtyo anatajwa kuwa mbioni kutua Singida United, aliyekuwa mchezaji wao wa zamani, Fred Felix Minziro, kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime, lakini pia Katibu Mkuu wa Wanajangwnai hao, Boniface Mkwasa.

Hata hivyo, pamoja na mipango yao hiyo, bado Yanga inakabikliwa na changamoto ya kifedha ambayo huenda ikaathiri hilo iwapo hakuna ‘kibosile’ anayeweza kujitokeza kuokoa jahazi.

Kikosi cha Yanga kwa sasa kipo chini ya kocha msaidizi, Shadrack Nsajigwa pamoja na kocha wa viungo, Noel Mwandila, huku makipa wakinolewa na Juma Pondamali

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU