FEBRUARI HII JAMANI, MMESHATAFUTA REFA?

FEBRUARI HII JAMANI, MMESHATAFUTA REFA?

1042
0
KUSHIRIKI

KABLA ya yote ningependa kwanza kuwasihi kitu kimoja ndugu zangu, mpaka leo dunia ikiwa na karne zaidi ya 20, hajawahi kutokea mfalme wa njaa.

Acheni utani kabisa na kitu kinachoitwa tumbo, ‘eni taim’ linaweza kukudhalilisha.

Tumbo bwana lina kisirani sana, usipokula, linakupa vidonda vya tumbo, ukila sana linavimba, ukila ovyo linakupa minyoo na kipindukipindu juu, nyie tumbo kitu kibaya sana.

Teh teh teh…. haya nyie oneni utani tu, we unafikiri yule mjamaa kilichomrudisha nini kama si tumbo? Ni tumbo hamna lolote pale, vidonda vilishaanza kumtafuna yule.

Unafanya mchezo nini? Eti oooooh sijui nimestaafu, mara tena sijui hao viongozi siwezi kufanya nao kazi tena, mara sijui nini nini huko… wewe bwana, maneno hayashibishi aisee.

Si huyo karudi, tena katinga na mjezi unaofanana rangi na wale wataalamu wa jadi halafu hana habari, chezea tumbo wewe… Teh teh teh….

Usia wangu kwa leo ndio huo jamani, sasa tusalimiane. Kwema? Teh teh teh… habari za weekend wadogo kwa wakubwa.

Mie niko poa ila wiki hii kidogo viganja vya mikono vinaniuma sana.

Si unajua tena nilipata kazi ya kufua mijezi ya wale Lipuli, basi nakwambia nimekutana na vumbi sio la nchi hii, hizi kazi hizi!

Sema ndio vile tena sina wakumlaumu, mwenyewe na jeuri yangu ndio niliona madaftari mazito, acha nihenyeke tu.

Mji huu bana, nisijifanye kujua kwingi mwisho wa siku nikaishia kwenye orodha ya Mkuu wa Mkoa, teh teh teh…. sore jamani, isije nikawa nimegusa nafsi za watu hapa.

Teh teh teh… ila kiukweli kama mambo yakienda hivi, nitaomba tenda ya kufua mikoti ya Segerea kule. Maana nitakuwa natupia povu la kiwango cha juu kabisa, teh teh teh…. orodha ile bwana!

Ngoja nirudi zangu kwenye soka tu. Naona joto linazidi kupanda aisee, si ndio tofauti pointi moja sio, basi kazi ipo mwezi huu wa Wapendanao.

Yaani kiutani utani ile mechi ndiyo itakayoamua bingwa msimu huu, mtu akipigwa pale vijana wa leo ndio wanaita ‘imekula kwako’, teh teh teh…

Na si hamna majeruhi huko, maana msije nipa visababu kama vya kule visiwani.. ooh sijui nani anaumwa, sijui ndio maana tukafungwa, mie nimeona jezi zimekuja full huku, kwahiyo kila kitu najua kiko fresh.

Teh teh teh…. tena nimekumbuka, hivi yule bwana mkubwa kashatafuta marefa watakaochezesha ile mechi?

Maana juzi kati hapa nilisikia chama cha marefa kimempa idhini yule bwana kusaka marefa, sasa ndio nataka nijue jamani, kashapata?

Teh teh teh…. au ndio atawarudia wale masheikh wa Zanzibar kule maana wale bwana wakishapiga dua, wanazima simu, hawataki stori zisizoeleweka tena.

Sasa ndio nauliza tu, bwana msemaji atawachukua wale? Teh teh teh… presha ya watani si mchezo aisee, tena ndio kama hivi watu wanataka kombe, mbona kazi itakuwepo.

Teh teh teh… mie acha niifikiche hii mijezi hapa nikijiandaa na shughuli hiyo. Na viti vya uwanjani si vimeshapigwa supa gluu vizuri ili lolote litakalotokea, tubaki na usalama wetu tu.

Enheeee nilitaka nisahau bana, yale majamaa ya Younde yamebeba Afcon aisee.

Yaani kuna wale mastaa wao walijifanya kuleta za kuleta wakasusa kuja walipoitwa, wakajua ndio wanatia gundu, kumbe wapi! Gundu wamejitia wenyewe tu!

Vijana wamekaza mpaka ndoo imeenda Cameroon, teh teh teh… halafu kitu cha ajabu sasa, wakati wao wakibeba taji la tano, mashabiki wao wengi ni wale wanaotoka kwenye taifa ambalo hata halijui ladha ya Afcon kwa miaka 30 sasa.

Teh teh teh… sore kumbe nagusa masilahi ya watu, sore sana wakuu ila tufanyeni kweli basi hata hii Afcon ndogo ya vijana tubebeni jamani.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU