JITOE KWA MWENZAKO, ACHA KUMVIZIA

JITOE KWA MWENZAKO, ACHA KUMVIZIA

976
0
KUSHIRIKI

UWAPO katika uhusiano ni sehemu mwafaka sana kumwonesha mwenzako ni kwa kiwango gani ana bahati ya kukupata wewe katika maisha yake.

Katika hili, unatakiwa uache kujitazama zaidi wewe na badala yake ujitoe kwa ajili yake ili aone raha, furaha na thamani ya kuwa na wewe katika maisha yake.

Unaishi vipi katika uhusiano wako? Unajitoa kweli kwa ajili ya kumpatia raha, furaha na amani mwenzako ama unafanya tu mambo kwa kumwangalia yeye anakufanyia nini?

Wapo watu wanaohesabu simu wanazowapigia wapenzi wao kwa siku. Wapo wengine wanajua jana na juzi ni nani alianza kumtumia ‘sms’ mwenzake. Watu wa hivyo wapo.

Wao kazi yao kubwa ni kuangalia mbona mimi namfanyia hivi yeye kwanini hanifanyii. Wapo katika mahusiano ila ni kama wapo katika mashindano.

Wewe ni miongoni mwa watu hao? Watu ambao badala ya kuwa bize kufurahia uhusiano wao, wenyewe wanajishughulisha zaidi na tabia za kishindani?

Na wewe una orodha ya vitu unavyomfanyia mwenzako na unasubiri na yeye akufanyie ili uendelee kumfanyia mengine mazuri?

Na wewe badala ya kufurahia ubora wa mwenzako uko bize kufafanisha ubora wako na madhaifu yake na kujikuta ukiumia kwa namna mambo yalivyo?

Niliwahi kusikia rafiki mmoja akilalamika juu ya mwenzake. Akionekana anachanganywa sana na mwenzake, rafiki yangu huyo alikuwa akisema:

“Jana nimempigia simu mimi, juzi niliomba mimi tukutane, leo hapana bwana. Inabidi na yeye anifanyie kama mimi kama kweli ananipenda na ananimisi.”

Na wewe una fikra hizi? Na wewe umekumbwa na ugonjwa huu wa kujitakia na kujiona una haki ya kufananisha matendo na maneno baina yako na mwenzako?

Ndiyo, ni kweli kila mmoja aliye katika mahusiano hupenda hali fulani ya ‘kusumbuliwa’ na mwenzake juu ya kuonana, kujuliana hali hata kutoka kwenda maeneo ya kufurahi.

Ila mbali na ukweli huu, hiki ni kitu cha kukufanya utake ushindani hata kama mwenzako japo hakwambii ila kila unalofanya anaonekana kufurahia na kuridhia?

Acha ushindani. Katika mapenzi mkitaka mshindane nani ni mbabe basi kuachana kwenu ndiyo kutaibuka mshindi. Walio katika mahusiano halisi hupenda kushindana kupeana raha na si kukerana.

Wanaopendana hasa na kujua vizuri majukumu yao, hujibidisha kuwafurahisha wenzao bila kuangalia wao wanafanyiwa nini kwa muda husika.

Ndiyo huwa hivi, ukianza kuhesabu unamfanyia matendo mazuri mangapi mwenzako naye anakufanyia nini, hapo unakaribisha ushindani utakaoleta mpasuko baina yenu.

Kuwa ‘busy’ kumfanya mwenzako afurahie uwepo wako katika maisha yake. Matendo yako bora kwake ni kitu ‘kitakachomroga’ na kumfanya akuone bora na wa thamani katika maisha yako.

Acha ushindani. Mapenzi ya watu waliopevuka akili hayajengwi kwa ushindani usio na maana. Watu waliofanikiwa katika mahusiano yao, huzingatia zaidi matendo mazuri kuliko kulipiza ujinga waliowahi kufanyiwa na wenzao.

Ukilipiza ujinga kwa mwenzako eti kwa sababu aliwahi kukufanyia, jua unaleta ufa hatari katika uhusiano wako. Ufa ambao utaleta shida na mateso katika mahusiano yako hata ukashindwa kupata raha inayostahili.

Ili kufurahia mahusiano na mwenzako yafaa uwe halisi. Acha kutaka kufanya mambo kwa kutegeana na badala yake hakikisha unatimiza majukumu yako vile inavyopasa.

Acha kufikiria unachofanya kisha yeye hafanyi, fikiria yote unayotakiwa kumfanyia mwenzako kisha yafanye kwa uhakika.

Mahusiano ya kutegeana hata siku moja hayawezi kukuletea furaha unayotaka. Mbali na kuwa kila siku badala ya kufurahia mahusiano yako utakuwa ‘busy’ kuangalia nini anafanya ambacho umefanya, ila pia utajikuta unaumizwa na mawazo kwanini hafanyi unayofanya.

Njia halisi ya kufurahia mahusiano yako ni wewe kuwa ‘busy’ kufanya majukumu yako kwa mwenzako na kwa uhakika, hali hiyo itamjenga mwenzako kuamini kuwa unampenda na kumjali na kumfanya baadaye naye afanye kama unavyofanya wewe.

Tatizo la wengi katika mapenzi ni kutaka  wenzako wawafanyie mambo mazuri wanayotaka bila kutengeneza misingi ya mambo hayo kutokea.

Bila kufikiri, unakuta mtu anataka kupigiwa simu kila muda na mwenzake, anataka kujaliwa na kubembelezwa bila kuangalia kiwango cha matendo ya maana anayomfanyia mwenzake.

Kama unataka mwenzako awe unavyotaka wewe, yafaa na inakubidi ‘ummwagie, wingi wa matendo mazuri mwenzako. Kila linalofaa kumfanyia we mfanyie kwa namna kubwa bila kuangalia kwa muda huu anakfanyia nini.

Kila mmoja anatakiwa kufahamu hili, mbegu haioti siku moja. Badala ya kukaa na kuangalia mwenzako anakufanyia nini baada ya wewe kumfanyia kitu fulani, shughulika na kupanda mbegu kwanza (kumfanyia vitendo vizuri).

Kitaalamu tunaamini matendo yanazungumza (yana nguvu) kuliko maneno, badala ya kukaa na kulalamika kwanini hafanyi unavyotaka, mfanyie matendo mazuri zaidi mwenzako kwa maana kwa kufanya hivyo unakuwa unatuma taarifa katika akili yake kuwa unavyomfanyia ndivyo na wewe unatakiwa kufanyiwa.

Haina maana kupoteza muda wako ukilalama. Lawama mbali na kuwa ni upotezaji wa muda ila pia zinafanya mwenzako asiwe na bashasha na wewe.

Hakuna binadamu anapenda kuonwa ni yeye tu ndiye mkosaji, acha kulalamika namfanyia matendo bora bila kuangalia nini anafanya.

Mahusiano mengi yamekuwa imara baada ya wahusika kuzama katika matendo ya kuwafurahisha wenzao bila kujali wenzao wanafanya nini kwa muda husika.

Pandikiza mbegu za matenado unayotaka kufanyiwa na mwenzako kwa kumfanyia matendo hayo mhusika. Binadamu ni kiumbe mwenye akili na uelewa.

Hata kama leo haoneshi kujali sana, ila kuna muda kila binadamu hutumia kutafakari matendo yake na matendo anayofanyiwa. Ni katika muda huo ambapo nafsi yake itamsuta na kuona ana jukumu zito la kukufanyia.

Furahia mahusiano yako kwa kutimiza majukumu yako kwa mwenzako. Kumvizia kimatendo mwenzako hakuna faida yoyote zaidi ya hasara ya kuishi maisha ya kusitasita (hesitation life).

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU