JKT RUVU IMEFUNGA HESABU ZA KUSHUKA DARAJA

JKT RUVU IMEFUNGA HESABU ZA KUSHUKA DARAJA

1481
0
KUSHIRIKI

NA ONESMO KAPINGA

LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara imebaki katika ushindani wa timu zitakazochukua ubingwa na zile zitakazoshuka daraja msimu huu.

Ni timu mbili za Simba na Yanga ndizo zenye nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa wa msimu huu, zinazoshika nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo.

Simba ndio wanaoongoza katika msimamo huo kutokana na pointi 62  baada ya kucheza michezo 27 wakiwa wameshinda michezo 19 wakitoka sare mara tano na kufungwa michezo mitatu.

Yanga wanashika nafasi ya pili kutokana na pointi 56 wakiwa wamecheza michezo 25 wakishinda mara 17, wakitoka mara tano na kupoteza michezo mitano.

Hata hivyo, nafasi ya timu itakayochukua ubingwa msimu huu inaonekana bado kutokana na ukweli kwamba, kati ya timu hizo moja inaweza kutwaa taji hilo.

 

Simba wameendelea kuongoza katika msimu huo kutokana na kucheza michezo mingi kuliko Yanga, lakini wakiwa na pointi tatu walizopewa na Kamati ya Saa 72 ya Shirikisho la Soka Tanzania Bara, iliyozua utata kwa takribani wiki tatu.

 

Pointi hizo ambazo Kamati ya Saa 72 iliipoka Kagera Sugar, ilitokana na malalamiko ya Simba kuwa Kagera ilimchezesha beki wao Mohamed Fakhi, aliyekuwa na kadi tatu za njano.

Na Simba wakiendelea kubaki na pointi hizo na wakashinda michezo yao mitatu iliyosalia, wataweza kuchukua ubingwa wa msimu huu.

 

Lakini Simba wakipoteza hesabu zao Yanga watakuwa na nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wao wakishinda michezo mitano iliyosalia.

Yanga wana nafasi ya kutetea taji lao, lakini waendelee kuomba  Simba wateleze katika michezo yao mitatu iliyosalia, kwani timu inayowafuatia Azam haina nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa msimu huu.

 

Azam wana shika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, kutokana na pointi 46 baada kucheza michezo 27 na wakishinda mitatu iliyosalia watakuwa na uwezo wa kufikisha pointi 55 huku Yanga tayari wana pointi 56.

Hata Kagera Sugar wakishinda michezo yao mitatu iliyosalia wanakuwa na uwezo wa kufikisha pointi 53 ambapo kwa sasa wana pointi 44, baada ya kucheza michezo 27.

Ushindani mwingine wa soka unaonekana katika timu tano zinazopigana kushuka daraja msimu huu, ambazo ni Mbao FC, Ndanda, Toto Africans, Majimaji na JKT Ruvu.

Mbao FC ambao walipanda daraja msimu uliopita hawako katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi hiyo, kwani inahitaji kushinda michezo yao mitatu iliyobaki huku ikisubiri matokeo ya mwisho ili kujihakikishia kubaki msimu ujao.

Timu hiyo inashika nafasi ya 12 kutokana na pointi 30 wakifuatiwa na Ndanda wanaoshika nafasi ya 13 kutokana na pointi 30.

 

Ndanda wamecheza michezo 28 wakishinda miwili iliyosalia itakuwa na uwezo wa kufikisha pointi 36 lakini itasubiri timu itakayowabeba kati ya hizo tano ambazo ziko kwenye hatari ya kushuka daraja, iwapo zinafungwa.

Toto Africans nayo haiko katika mazingira salama ya kubaki kwenye ligi hiyo, kutokana na inahitaji kushinda michezo yake minne ili ijihakikishie kucheza msimu ujao.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Toto Africans inashika nafasi ya 14 kutokana na pointi 26 na ikishinda minne iliyosalia itakuwa na uwezo wa kufikisha pointi 38.

Majimaji inayoshika nafasi ya 15 inahitaji miujiza kwani iko katika mstari mwekundu wa kushuka daraja ambayo ina pointi 26 baada ya kucheza michezo 27.

Timu hiyo ikishinda michezo mitatu iliyosalia itakuwa na uwezo wa kufikisha pointi 35 huku ikisubiri hadi mchezo wa mwisho ili kuona kama itabaki msimu ujao.

JKT Ruvu inazibeba timu 15 zinazoshiriki ligi hiyo, kwani hadi sasa inaonekana imefunga hesabu za kushuka daraja msimu huu.

Pamoja na timu hiyo kusaliwa na michezo mitatu hesabu zao za kubaki kwenye ligi hiyo hazitaweza kukamilika kutokana na watakuwa na uwezo wa kufikisha pointi 29, ambazo hazitawawezesha kubaki.

JKT Ruvu tayari iko kwenye kundi la timu tatu zikakazoshuka daraja huku ikizisubiri nyingine mbili ambazo ziko kwenye mstari mwekundu wa kushuka.

Tukutane Jumatatu ijayo

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU