KAGERE, BOCCO VITANI SIMBA

KAGERE, BOCCO VITANI SIMBA

2856
0
KUSHIRIKI

NA SAADA SALIM


STRAIKA wa kimataifa wa Simba, Meddie Kagere, ameingia vitani na mzawa, John Bocco, katika suala zima la ufungaji mabao, ikiwamo staili ya uchekaji na nyavu.

Kagere ameifungia Simba mabao matatu katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, huku mawili akifunga kwa kichwa.

Baada ya kuona jinsi mshambuliaji mwenzake huyo anavyowateka mashabiki na wanachama wao kwa kasi yake hiyo ya mabao, hatimaye Bocco naye amecharuka na kumjibu nyota huyo raia wa Rwanda.

Kuonyesha jinsi asivyotaka utani katika kazi yake hiyo, Bocco juzi aliingia katika vita kwa kumjibu Kagere baada ya kufunga mabao mawili, yote akiyaweka kimiani kwa kichwa katika mchezo wa kirafiki dhidi ya AFC Leopards kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambao Wekundu wa Msimbazi walishinda mabao 4-2.

Tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara, Bocco amecheza mechi mbili bila ya kufunga bao, huku Kagere akifunga matatu.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Kagere alifunga bao lingine kwa kichwa kuipa timu yake ya Taifa ya Rwanda bao la kufutia machozi katika kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Ivory Coast.

Uwapo wa mastraika hao, Kagere na Bocco, unaifanya safu ya ushambuliaji ya Simba kuwa na uhakika wa kufunga mabao mengi, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems, akionekana kuwa na furaha kutokana na wachezaji wake hao kufanya vizuri.

Akizungumza na BINGWA baada ya mchezo dhidi ya Leopards, Bocco alisema anachokiangalia kwa sasa ni kushirikiana na wenzake kuhakikisha wanafanya vizuri kwa kila mechi iliyopo mbele yao.

Alisema msimu huu wapo vizuri, akijivunia umoja na ushirikiano na wachezaji wenzake, akiamini utawafikisha katika kile kinachotarajiwa na Wanasimba, yaani kutetea taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

“Kikosi chetu kipo vizuri, kwa ushirikiano na umoja wetu tutafikia malengo, tunahitaji kupata sapoti kwa mashabiki kuhakikisha hatutawaangusha na kuhakikisha tunatwaa taji hilo pamoja na kufanya vizuri katika michuano mingine,” alisema Bocco.

Naye Kagere alisema alivyokiona kikosi cha timu yake kipo vizuri na amekuja Simba kufanya kazi na kuhakikisha atashirikiana na wenzake ili kuipa timu yake matokeo mazuri.

“Mashabiki watarajie makubwa, napata ushirikiano mzuri kutoka kwa wenzangu, ukizingatia katika safu yetu ipo vizuri na tutahakikisha hatutawaangusha Wanasimba,” alisema Kagere.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU