KASEKE KUMFUATA BANDA AFRIKA KUSINI

KASEKE KUMFUATA BANDA AFRIKA KUSINI

6348
0
KUSHIRIKI

SALMA MPELI NA ZAINAB IDDY


KIUNGO wa timu ya Singida United, Deus Kaseke, yupo mbioni kumfuata Abdi Banda, anayecheza Ligi Kuu ya nchini Afrika Kusini, baada ya kupata dili kutoka klabu ya Highlands Park, itakayoshiriki ligi hiyo.

Kaseke anatarajiwa kujiunga na timu hiyo iliyopanda daraja msimu uliomalizika, baada ya kumalizika kwa mazungumzo baina ya Highlands Park na Singida, ambako bado ana mkataba wa mwaka mmoja.

Awali Kaseke, aliyewahi kuichezea Yanga na Mbeya City kwa vipindi tofauti, alitajwa kuwa huenda angeondoka na kocha wake, Hans van der Pluijm, aliyetimkia Azam FC kuinoa kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Akizungumza na BINGWA jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Singida United, ambaye pia ni Mkurugenzi wa klabu hiyo, Festo Sanga, alisema ofa ya timu inayomhitaji Kaseke tayari imeshafika mezani, hivyo kilichobaki ni wao kukaa chini na kuangalia kama itawafaa.

“Kaseke amepata ofa kutoka Afrika Kusini ambako timu ya Highlands Park iliyopanda Ligi Kuu ndiyo inamhitaji, muda wowote uongozi wa Singida utakutana na meneja wa mchezaji ili kuangalia maslahi ya mchezaji na timu,” alisema.

Kwa upande wa Meneja wa Kaseke, Milamo William, aliliambia BINGWA kuwa, taarifa za mchezaji wake kupata timu anazo, lakini muda wa kuweka wazi jambo hilo bado haujafika.

“Hizo taarifa zipo, lakini siwezi kuweka wazi kwa sasa kwa sababu Kaseke bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Singida ambao ndio wana mamlaka ya kulielezea jambo hili kwa undani,” alisema Milamo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU