KATWILA: TUPO TAYARI KUPAMBANA KIMATAIFA

KATWILA: TUPO TAYARI KUPAMBANA KIMATAIFA

5124
0
KUSHIRIKI

NA SAADA SALIM

KOCHA mkuu wa timu ya Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, amesema kikosi chake kipo tayari kupambana katika michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Mtibwa Sugar ndio watakaowakilisha katika michuano hiyo baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) maarufu Kombe la FA, huku Simba wakijiandaa na Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Akizungumza na BINGWA jana, Katwila, alisema licha ya Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf) kutotangaza wapinzani wao, lakini kikosi chake kipo fiti kufanya vizuri.

“Caf bado hawajapanga ratiba wala  hatuwafahamu wapinzani wetu, lakini kikosi chetu kipo tayari kukutana na timu yoyote ambayo tutapangiwa,” alisema.

Aidha, alisema licha ya baadhi ya wadau wa soka kutoipa timu yake nafasi kubwa ya kufanya vizuri kimataifa, lakini wao wanajua kitu watakachofanya na kuwashangaza wengi.

Hata hivyo, alieleza kuwa miaka ya nyuma waliposhiriki michuano ya kimataifa hawakufanya vizuri ikiwamo kutokucheza mechi ya marudiano dhidi ya timu ya Santos ya nchini Afrika Kusini mpaka kufungiwa na Caf, lakini hawataki hayo yajirudie.

“Kufanya vizuri kwa timu yetu katika ligi kunatupa mwanga lakini pia mapungufu tutayafanyia kazi kabla ya kuanza kwa michuano hiyo, miaka ya nyuma tulifanya vibaya lakini sasa tupo tayari kwa mapambano,” alisema Katwila.

Mtibwa ilifungiwa miaka mitatu kutokana na kushindwa kwenda kucheza mechi ya marudiano na Santos mwaka 2003, ikiwa ni baada ya kufungwa mabao 3-0 nyumbani katika mchezo wa awali.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU