KOCHA MPYA YANGA: RAYON NIACHIENI

KOCHA MPYA YANGA: RAYON NIACHIENI

8531
0
KUSHIRIKI

NA WAANDISHI WETU


 

KOCHA wa Yanga, Zahera Mwinyi, amesema amezinasa siri zote za wapinzani wao, Rayon Sports ya Rwanda, hivyo amewataka mashabiki wa timu hiyo kutulia na  kumwachia kazi ya kuwamaliza Wanyarwanda hao.

Yanga watakutana na Rayon Sports katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho, huku wakiwa na kumbukumbu ya kupigwa mabao 4-0 na USM Alger ya Algeria wiki iliyopita.

Kipigo hicho kinaifanya Yanga kuburuza mkia katika Kundi D la michuano hiyo, timu nyingine ikiwa ni Gor Mahia ya Kenya.

Akizungumza na BINGWA jana kuelekea mchezo huo wa kesho, Mwinyi alisema amewaona wapinzani wao kupitia mikanda ya video ambayo timu hiyo ilicheza dhidi ya Gor Mahia na kugundua udhaifu wao ulipo.

“Ni timu nzuri, si ya kuibeza kabisa, nina imani kama wachezaji wangu wataondoa mawazo yao ya nje ya uwanja, tunaweza kufanya vizuri na kushinda keshokutwa (kesho),” alisema Mwinyi.

Alisema Rayon wana washambuliaji wazuri pamoja na viungo, lakini hiyo haiwafanyi washindwe kupata ushindi mbele ya Wanyarwanda hao ambao wamekuwa na mwenendo wa kusuasua kwenye Ligi Kuu nchini kwao.

“Mpira ni mchezo ambao hautabiriki, lakini pia una matokeo matatu, nina imani kwa maandalizi mazuri ambayo tunaendelea kuyafanya, vijana wangu wana kila sababu ya kuibuka na ushindi na kurejesha matumaini ya kucheza nusu fainali,” alisisitiza Mwinyi.

Wakati Mkongomani huyo akitamba hayo, kikosi cha Rayon Sport kwa sasa kinapita katika wakati mgumu baada ya kushindwa kupata matokeo mazuri kwenye michezo yake ya Ligi Kuu nchini Rwanda kama ilivyo kwa Yanga ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kikosi cha Rayon kinachonolewa na Ivan Minnaert, kwa sasa kinashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Rwanda, huku kikiwa kimecheza mechi 19 na kukusanya pointi 36.

Kwenye michezo mitano waliyocheza hivi karibuni, wameshindwa kupata ushindi na badala yake wakiambulia sare tu, huku Kigali FC ikiongoza ligi hiyo baada ya kukusanya pointi 42.

Licha ya kupita kwenye nyakati mbaya kwa sasa, Nahodha wa Rayon, Ndayishimiye Eri Bakame, amesema kamwe hawatakubali kupoteza mchezo huo wa kesho.

Alisema japo Yanga ina wachezaji wenye uzoefu, wanatambua nyota wote wanaopaswa kuchungwa kwenye mchezo huo.

“Tumeangalia CD za mechi zao, pia kupata taarifa za wachezaji wa timu hiyo ambao tutakuwa nao makini kuhakikisha hawatatusumbua,” alisema.

Bakame aliwataja mastraika tishio wa Yanga kuwa ni Obrey Chirwa ambaye hatacheza mchezo huo, Ibrahim Ajib na Yussuph Mhilu ambao walionyesha kiwango kizuri katika mchezo wa marudiano dhidi ya Township  Rollers ya Botswana.

Kwenye michuano hiyo, Yanga inatakiwa kushika nafasi mbili za juu kwenye kundi lake ili iweza kutinga robo fainali ambapo inahitaji kushinda angalau mechi nne na kutoa sare mbili tu.

Katika hatua nyingine, kikosi cha Yanga jana kiliendelea na mazoezi kuwawinda Rayon kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambao ni Kelvin Yondani, Youthe Rostand, Thabani Kamusoko, Vincent Andrew ‘Dante’, Obrey Chirwa, Gadiel Michael, Pato Ngonyani, Rafael Daudi, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Hassan Kessy, Yusuph Mhilu, Amissi Tambwe, Geoffrey Mwashiuya, Yohana Nkomola, Pius Buswita, Emmanuel Martin na wengineo wa Yanga B.

HABARI HII IMEANDIKWA NA HUSSEIN OMAR, ZAITUNI KIBWANA NA SAADA SALIM

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU