LULU ATOKA GEREZANI MASTAA WAMPOKEA, MAMA KANUMBA ALAZWA

LULU ATOKA GEREZANI MASTAA WAMPOKEA, MAMA KANUMBA ALAZWA

8439
0
KUSHIRIKI

 

NA CHRISTOPHER MSEKENA


 

 

ELIZABETH Michael maarufu kama Lulu ambaye ni mwigizaji nyota nchini, amebadilishiwa kifungo chake kutoka kile cha miaka miwili jela alichokuwa anakitumikia toka Novemba 13, mwaka jana mpaka kifungo cha nje kwa amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam.

Katika taarifa iliyotolewa jana na Jeshi la Magereza Tanzania, ilieleza kuwa Lulu ambaye alikuwa mfungwa namba 1086/2017, katika Gereza la Segerea Dar es Salaam, alibadilishiwa adhabu hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Magereza sura ya 58 kifungu Namba 49 (1), (2), (3), kinachosema mfungwa yeyote isipokuwa wa konyongwa au wa maisha baada ya kupokewa gerezani hupata msamaha 1/3 ya kifungo chake.

Taarifa hiyo iliendelea kubainisha kuwa Aprili 26, mwaka huu, katika kuadhimisha miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45 (1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa msamaha robo kwa wafungwa wote waliokuwa na sifa akiwamo Lulu, hivyo kutakiwa kutoka gerezani Novemba 12, mwaka huu.

Hivyo basi Lulu, aliachiwa Mei 12 mwaka huu kwenda kutumikia kifungo cha nje kwa amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa kifungu namba 3 (2) (a) cha sheria ya Huduma kwa Jamii ya mwaka 2002, wafungwa ambao vifungo vyao havizidi miaka mitatu hunufaika na utaratibu huo, kwa kutumikia kifungo cha nje kwa kufanya kazi au shughuli zisizo na malipo kwa manufaa ya jamii.

ILIKUWAJE?

Lulu alihukumiwa kwenda jela miaka miwili kwa kosa la kumuua bila kukusudia msanii wenzake, Steven Kanumba, Aprili 7, mwaka 2012, hukumu hiyo ilisomwa Novemba 13, mwaka jana na Jaji wa Mahakama Kuu, Samu Rumanyika, baada ya kusikiliza utetezi wa pande zote mbili.

MASTAA WAMPOKEA

Taarifa za Lulu kubadilishiwa adhabu na kuanza kutumikia kifungo cha nje mpaka Novemba 12 mwaka huu, atakapokuwa huru kabisa zimepokewa kwa furaha na mastaa mbalimbali.

Wafuatao ni miongoni mwa mastaa waliotumia mitandao mbalimbali ya kijamii kumpongeza na kumtia moyo Lulu kwa hatua hiyo muhimu kuelekea kuwa huru.

Wema Sepetu

Kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika ‘Welcome Back Baby’.

RIYAMA ALLY

Naye kupitia ukurasa wake wa Instagram alimshukuru Mungu kwa kuandika “Alhamdulilah asante Mwenyezi Mungu kwa kila jambo, Mungu ni mwema sana, akuvushe hilo na jingine Amin Rabila Alamina.”

STEVE NYERERE

Katika ukurasa wake wa picha alitoa neno la busara akisema: “Ni jambo la kushukuru sana kwani kila pito naamini Mungu yupo pamoja nawe Lulu, nichukue nafasi hii kwa dhati kabisa kumshukuru Mh Rais John Pombe Magufuli kwa msamaha huu, naamini umefanya jambo jema sana Rais wangu, niipongeze Mahakama pia na wadau wote mliokuwa mnamwombea mwenzetu kutoka, familia njoo Lulu tujenge tasnia yetu.

MAMA KANUMBA

BINGWA lilimtafuta mama mzazi wa marehemu Steven Kanumba ili kupata mtazamo wake juu ya hatua hiyo ya hukumu ya Lulu, naye alidai tumwache kwa muda kwani yupo hospitali amelazwa akisumbuliwa na ‘presha’.

 

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU