MAPENZI HUKUFANYA KUWA HIVI

MAPENZI HUKUFANYA KUWA HIVI

1037
0
KUSHIRIKI

NA RAMADHANI MASENGA


 

BINTI mmoja aliniandikia ujumbe akinieleza juu ya madhila anayopitia katika uhusiano wake. Alisema yeye ana mpenzi anayempenda sana.

Kutokana na kumpenda huko, mbali na kuhitaji kuwa naye karibu muda mwingi ila huwa tayari kufanya lolote la maana la kumfurahisha mwenzake.

Kwa hali hiyo, akajikuta hata akiamua kukubali ushauri wa mwenzake kubeba ujauzito angali wakiwa bado hawajaingia katika ndoa.

Alisema alifanya hivyo kwa sababu mbili. Kwanza, kwake ilikuwa fahari kubwa kubeba mimba ya mtu anayempenda ila pili, alifanya hivyo ili kumfurahisha mwenzake.

Pamoja na kufanya yote hayo, binti anasema mwenzake hamjali, hampigii simu mpaka apige yeye. Pia hataki hata kidogo kuzungumzia suala la ndoa na zaidi haoneshi fahari ya kuwa naye katika maisha jambo linalomfanya wakati mwingine apate sononeko.

Sasa binti akauliza. Mtu wa namna hii kweli ana mapenzi ya kweli? Wengi mtashangaa swali la binti huyo. Mtashangaa kwa sababu dalili zinaonesha wazi kwamba mwenzake hana mapenzi ya kweli kwake.

Ila msimshangae binti huyo. Mapenzi ya kweli yako hivyo. ukimpenda sana mtu hata kukupelekea kuamini kwamba yeye ndiye mtu pekee mwenye kufaa sana katika maisha yako, huwa ni ngumu sana kuamini kwamba hakupendi hata kama anafanya matendo ya kijinga yenye kutia mashaka upendo wake juu yako.

Mapenzi yako hivyo. Mapenzi yanakupa sababu ya kusubiri na kuangalia matokeo mengine. Mapenzi ya kweli kwa wengine yanawazuia kuwafikiria wenzao vibaya hata kama ni kweli wanafanya mabaya.

Ni dhahiri mtu akiwa haoneshi kukuheshimu, kukujali, kukusikiliza na kutekeleza mengi unayotaka ayatekeleze, ni dalili za kutokuwa na mapenzi nawe kwa kiwango stahili. Ila yote hayo kafanyiwa huyo binti, bado anauliza juu ya mapenzi halisi ya mwenzake juu yake.

Haulizi akiwa hajui. Anauliza akitaka kusikia kitu tofauti kidogo kutoka kwa mwingine. Anataka mtu atakayemwambia kwamba mwenzako anakupenda ila kuna mambo tu labda hayako sawa.

Neno la namna hii analitaka sana. Analitaka kwa sababu litampa faraja na nguvu ya kuendelea kuamini mapenzi kwa mtu anayempenda na kumjali.

Mtu wa namna hii kumshauri tofauti na anavyotarajia inahitaji busara na utaalamu. Kinyume na hapo ataona hujui kitu. Ndiyo ataona hujui kitu hata kama utakalomwambia ni la ukweli.

Mapenzi ni upofu. Mtu akiwa katika usingizi wa mapenzi gololi huiona ni dhahabu. Sasa mtu wa namna hii ambaye anaamini mtu aliye naye ndiye sahihi ukimwambia kwamba si sahihi atakuona mjinga.

Atakuona mvunja mapenzi ya watu bila kuangalia wala kupima juu ya yote ya ovyo anayotendewa. Kuna kesi nyingi mtaani kuhusu watu waliotoa ushauri kwa fulani na kisha wakachukiwa.

Jirani anaweza kumwona rafiki yake anavyoteseka katika mapenzi, hajaliwi, anadhalilishwa na kutukanwa. Kwa nafsi yake kunjufu iliyojaa upendo anaweza kuamua kumpa ushauri mwenzake wa kumuepuka mhusika.

Ila kutokana na ulevi wa mapenzi mwenzako alionao, hauchukulii huu kama ushauri ila anaona kama uchonganishi.

Badala ya kukaa na kutafakari kwa kina juu ya usahihi wa kilichozungumzwa, yeye anaenda kumwambia mhusika yote aliyoambiwa. Baada ya hapo kifuatacho ni ugomvi.

Mapenzi ni kitu kinachohitaji umakini na hesabu sana. Si mapenzi ya hisia za mtu kwa mtu tu ila hata mapenzi ya chama A kwa chama B.

Mashabiki ama wanachama wa chama A wanaweza kumtukana kiongozi wa chama B kwa hoja fulani na kuuaminisha umma kuwa hafai kabisa.

Ila siku ikitokea akatoka chama A na kwenda chama B, wale wale waliokuwa wakimtukana na kumkashifu watamvika joho la utukufu na umahiri.

Mapenzi ndivyo yalivyo. Kwa sababu ya mapenzi inakuwa rahisi sana kuona doa kwa mwenzako aliye mita kumi, kuliko doa lililo katika shati lako ulilovaa. Hayo ndiyo mapenzi.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU