MAPENZI YANA ALAMA ZAKE, ZIDISHA UMAKINI

MAPENZI YANA ALAMA ZAKE, ZIDISHA UMAKINI

1276
0
KUSHIRIKI

Na Ramadhani Masenga

HUTAKIWI kukurupuka kuingia katika mapenzi. Inabidi uwe makini katika kumsoma mtu tabia zake kisha ndio uamue kuwa naye ama la.

Mapenzi ya fulani juu yako hayatakiwi kuonekana katika maneno tu. Kila mmoja anaweza kusema lolote. Mdomo umekuwa nyezo muhimu ya kufanya watu waamini vile tunavyotaka wao waamini hata kama hatumaanishi. Mapenzi hayatakiwi kupimwa kwa namna anavyosema tu.

Mapenzi yake kwako, yanatakiwa kujitafsiri yenyewe kupitia tabia na matendo yake. Jaribu kufikiria, kama angekuwa bubu usingeamini kama anakupenda kisa tu hasemi?

Unaweza kumjua anayekupenda kwa dhati hata kama hajawahi kukwambia hivyo. Sasa badala ya kubabaika na fulani anavyosema kuwa anakupenda, jiulize unauona upendo wake katika maisha yako?

Watu wengi wana wasiwasi na mpenzi ya wenzao juu yao, wanasema wanaambiwa wanapendwa ila matendo ya wahusika ni tofauti sana na mtu mwenye upendo anavyotakiwa kuwa.

Mwenye upendo wa dhati ni mara chache sana unaweza kumtilia shaka juu ya dhamira yake kwako. Japo kuna wakati anaweza kukupa wasiwasi, labda kutokana na misongo ya maisha, ila matendo yake mengi yatampambanua namna anavyokupenda na kukuhitaji.

Mapenzi ni kama jani kavu ukilikanyaga ni lazima litoe sauti. Mwenye upendo wa dhati juu yako anaweza kuwa mjinga na asiye jitambua, ila utahisi tu namna anavyokupenda kutokana na aina ya matendo yake.

Mapenzi sio hisia zinazoweza kujificha kwa muda mrefu. Mtu mwenye hisia za mapenzi hulazimishwa na hisia hizo kufanya matendo mazuri kwa mhusika.

Watu wengi wanateseka katika mahusiano kwa sababu wamekariri kuwa mtu mwenye kukupenda atakupa pesa na ahadi tamu tamu.

Dhana hii imefanya matapeli wengi wa mapenzi kutumia udhaifu wa imani hii kupenya katika maisha ya wengi.

Pesa anaweza kukupa yeyote hata ambaye hakupendi ikiwa tu ana lengo fulani la kutimiza katika maisha yako.

Mtu mwenye upendo wa dhati juu yako utamuona namna alivyo wa dhati juu ya matendo yake juu yako. Hafanyi mazuri leo tu, ila atafanya kila siku kwa sababu anasukumwa na nafsi yake kufanya hivyo.

Mtu mwenye kuigiza kukupenda, atakujali leo na kesho ila kesho kutwa hawezi tena kwa sababu anajilazimisha ila halazimishwi na nafsi yake.

Watu wengi wanalia kisha wanasema mapenzi mabaya. Hapana. Mapenzi ni raha na amani. Hakuna anayeuia kwa ajili ya mapenzi. Wanaolia na kuumia ni kwa sababu wako na watu wenye kuigiza mapenzi ila hawana mapenzi ya dhati juu yao.

Mwenye mapenzi ya dhati hawezi kumliza mwenzake. Amtaliza vipi mtu ambaye anamuona ni maalumu na wa kipekee katika maisha yake?

Kukosekana kwa mapenzi ndipo huleta machafuko. Mtu hawezi kujiua  akigundua anapendwa sana ila akigundua hapendwi anaweza kujidhuru. Mapenzi sio mabaya. Uongo wa kuigiza mapenzi ndio ubaya.

Mapenzi yanajenga daraja baina ya watu wenye asili, viwango na maono tofauti. Mapenzi yameweza kuwafanya watu wa mataifa mbali mbali wasahau tofauti ya asili yao na kuungana. Mapenzi yamewafanya watu wa dini mbili tofauti kuishi pomoja na kujiona ni wamoja. Mapenzi yanawaunganisha wanachama mahasimu wa vyama viwili tofauti vya siasa na kujiona ni wamoja.

Ili usiwe mhanga wa kulia kwa kukosa mapenzi mwafaka kwa mtu, kuwa makini kabla hujakubali kuingia katika mahusiano. Mpenzi yana alama zake. Mtu mwenye kukupenda hahitaji aongee sana, matendo yake na tabia yake juu yako itatafsiri kiwango cha mapenzi alicho nacho juu yako.

Badala ya kubabaika na mwonekano au hali yake ya kimaisha na kukimbilia kuwa naye, jifunze kuwa na subira. Cheza na akili yake ujue ni kwa kiwango gani yuko tayari kuwa na wewe katika maisha yake. Mchunguze na utambue ni kweli anakupenda kama anavyosema ama anasema anakupenda kwa sababu ya tabia yake ya kunywa mchuzi wa pweza.

Huyo mwanamke anayesema anakupenda, ni kweli ana maanisha ama anasema anakupenda kwa sababu anajua baada ya kuwa na wewe utampunguzia mzigo wa gharama katika maisha yake.

Usibabaike na mtu, chunguza tabia yake, gundua chamira iliyojificha katika kauli yake ya kudai anakupenda. Kisha baada ya kujua kila kitu toka kwake, fanya uamuzi unaoamini ni muafaka katika maisha yako.

Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia( Psychoanalyst)

ramadhanimasenga@yahoo.com

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU