MASTAA WAMLILIA SAM WA UKWELI, RIDHIWAN ASEMA YAKE

MASTAA WAMLILIA SAM WA UKWELI, RIDHIWAN ASEMA YAKE

6127
0
KUSHIRIKI

CHRISTOPHER MSEKENA Na PATRICIA KIMELEMETA


MWILI wa staa wa Bongo Fleva, Salim Mohamed ‘Sam wa Ukweli’, unatarajia kuzikwa leo Kiwangwa, Bagamoyo, baada ya kufariki dunia usiku wa kuamkia jana akiwa Hospitali ya Sinza Palestina, Dar es Salaam.

Mastaa mbalimbali katika kiwanda cha burudani wameguswa na kifo hicho, ambacho meneja wake, Amri The Business ameliambia BINGWA kimetokana na malaria na UTI, huku  mwili wake ukitarajiwa kuagwa leo katika Hospitali ya Mwananyamala, kabla ya kusafirishwa kwenda Bagamoyo alikojenga nyumba yake kwa mazishi.

“Jana (juzi) usiku alikwenda studio maeneo ya Mabibo kuna nyimbo mpya alikwenda kumalizia, majira ya saa mbili usiku prodyuza Bababyser, akanipigia simu akaniambia Sam anaumwa hivyo niende studio nikiwa na mkewe (Sam),

“Nikajiandaa, prodyuza akanijulisha tena kuwa wanampeleka Hospitali ya Sinza Palestina, nikiwa natoka nyumbani Ilala nikaambiwa tayari amefariki, nikaenda mpaka hospitali, nilipofika nikaanza taratibu za kuwajulisha ndugu zake kama wajomba kabla ya kuuchukua mwili na kuupeleka Mwananyamala,” alisema Amri.

Katika msiba uliowekwa Tandale kwa mjomba wa Sam wa Ukweli, mkewe alishindwa kuhudhuria kutokana na kuzimia mara kadhaa, hivyo kubaki nyumbani kwa mama yake, Yombo, Dar es Salaam.

Miongoni mwa mastaa waliotoa pole zao huku wakionyesha kushtushwa na taarifa hizo ni Diamond Platnumz, Profesa Jay, Aslay, Ali Kiba, Snura, Harmonize, Billnas, Jux, Nandy, Aslay, Kala Jeremiah na wengine wengi.

Naye Mbunge wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete, ameliambia Papaso la Burudani kuwa, kifo hicho kimemshtua, kwa sababu Sam wa Ukweli aliwahi kumpigia debe katika kampeni za kuwania ubunge kwenye jimbo hilo.

Ridhiwan alisema mwaka 2014, Sam wa Ukweli alitunga wimbo wa Kikwere unaoitwa Mama K Mlongele Tata, kwaajili ya kuhamasisha wananchi kuichagua CCM katika uchaguzi wa marudio jimboni hapo.

“Sam wa Ukweli alitunga wimbo wenye lugha ya Kikwere uliojulikana kwa jina la Mama K Mlongele Tata’, ambao ulimaanisha mama Kikwete mwambie baba mtoto amekua.

“Wimbo huo iliweza kuwahamasisha wananchi wengi ambao waliweza kuja kwenye mikutano yangu ya kampeni kwa ajili ya kusikiliza sera za CCM na ahadi zetu, hivyo Sam alikuwa kama ndugu yangu,” alisema Ridhiwani.

Sam wa Ukweli ambaye ni mume na baba wa mtoto mmoja wa kike anayeitwa Betty, alianza kuziteka chati za muziki ndani na nje ya nchi mwaka 2010, kwa nyimbo kama Sina Raha, kisha Hata kwetu Wapo, Loney, Kisiki, Samaki, Sweet Love  na Milele zikifuatia.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU