MIAKA MINNE? LIONEL MESSI ANA NINI KIPYA?

MIAKA MINNE? LIONEL MESSI ANA NINI KIPYA?

896
0
KUSHIRIKI

LIONEL Messi, mchezaji bora duniani, amekubali kutoliacha kasri lake la kifalme la Nou Camp baada ya kukubali kusaini mkataba mpya wa kubaki Barcelona hadi mwaka 2021.

Siku chache baada ya kusherehekea miaka yake 30 ya kuzaliwa, mchawi wa soka ameibariki ndoa yake na Barca. Ameahidi kuwa nao katika shida na raha nyingine.

Umri aliofikia Messi ndio ule ambao mastaa wengi wa soka huanza kupungua makali yao uwanjani.

Ndio wakati ambao hukutana na hali ngumu isiyozoeleka kirahisi. Wengine hushindwa kabisa na miili yao huanza kugoma huku akili ikilazimisha kuendelea kusakata soka.

Wengine Mungu aliwasaidia wakaweza. Na si kwa muujiza tu, bali waliamua sasa wapunguze kukimbia kimbia hovyo na kufanya machache ya muhimu ili waendelee kung’ara.

Messi ni mmojawapo wa wachezaji ambao kadiri umri unavyozidi kusonga, yeye anajipunguzia majukumu. Ila tunachosubiri kukiona msimu ujao atafanya nini kipya tofauti na yale tutakayoyafahamu hadi kufikia uamuzi wa kusaini mkataba wa miaka minne? Ana maajabu gani mengine ya kutufanya tumsubiri?

Mosi, tutegemee kumwona La Pulga akibadili eneo lake la kujidai uwanjani kutokana na umri wake.

Miaka saba iliyopita, Messi akiwa na umri wa miaka 20, alitumika kama winga-mshambuliaji au wakati mwingine alicheza karibu na lango kwa ajili ya kufungua minyororo ya ulinzi. Wakati ule ulishapita, sasa hivi umri wake umeshasogea na ile kasi hana tena.

Tumtegemee Messi atakayetumia ule uwezo wake usiochuja milele kwa kuwapokonya mabeki akitokea juu kidogo ya dimba. Hapa sasa tutamshuhudia Messi akirudi kwenye asili yake, yaani namba 10.

Usipate shida kung’amua iwapo Messi atafurukuta kwenye kiungo cha kati kisa alikuwa mshambuliaji, hivyo ‘kufanya hivyo kazi ya kiungo wa kati hataiweza.’

Messi uwezo wake wa kukokota mpira hata anapotokea mbele ya viungo wawili (double pivot) katika mfumo wa 4-2-3-1 ni mkubwa. Inategemea pia kama Ernesto Valverde atapenda kuutumia.

Na si katika mfumo huo, tusubiri kumfaidi Messi kwenye mfumo wa 4-3-3 iwapo tu Barca watakuwa na viungo wawili imara kiulinzi, kariba ya Marco Verratti wa PSG.

Tusubiri kumwona Messi ambaye hatatumia mbio sana bali atakuwa akifanya kazi ya Andres Iniesta, kutambua wapi na kwa wakati gani unaofaa kutumia kasi yake. Hatakuwa na ule moto aliozoeleka lakini atakimbia inapobidi na bado akawa na balaa.

Tutegemee kumuona Messi atakayeongeza nguvu ya mabao Barcelona. Messi aliletwa duniani na kuambiwa wazi rafiki yake kwenye soka ni nyavu.

Barca ina Luis Suarez na Neymar ambao wanafunga mabao ya kutosha tu. Barca inamtaka Ousmane Dembele wa Dortmund, ikiwa na maana wanataka mtu mwingine wa kufunga. Messi atakayecheza kiungo atakuwa akisaidia kuongeza idadi ya mabao hayo. Vuta picha ya safu ya ushambuliaji ya Barca yenye watu hao wanne itakuwaje.

Msimu uliopita La Pulga alicheza nafasi ya kiungo na ushambuliaji, akawa na majukumu makubwa na bado akaweza kufunga mabao 54 ndani ya mechi 52. Vuta picha mabao atakayofunga Messi na yale ya Suarez, Neymar na Dembele…iwapo atasajiliwa.

Kitakachobadilika ni aina ya mabao atakayofunga Messi.

Messi wa msimu ujao atakuwa anachelewa sana kufika golini lakini hatazuiliwa kufunga. Nenda kalitazame bao la ushindi alilowafunga Real Madrid Aprili mwaka huu utaelewa zaidi.

Kurudishwa safu ya kiungo kutamfanya Messi acheze mpira wa uhuru na kuisaidia Barca iwe na soka la utulivu katikati, japokuwa ni ngumu kwa wengi kuamini mshambuliaji ataweza kuwa kiungo bora.

Lakini tukumbuke huyu ni Messi mwenye uwezo wa kutandaza pasi za uhakika. Messi ambaye msimu uliopita alikuwa na wastani wa kutengeneza nafasi 2.19 ndani ya dakika 90 kwenye mechi za La Liga. Ufundi wa kupenyeza pasi za uhakika ndio utakaomfanya awe kiungo mchezeshaji wa kiwango cha dunia.

Uwezo wa kutuliza tempo ya mchezo itamfanya Messi awe hatari zaidi. Katika kitu ambacho Messi anakiheshimu ni namna ya kuwachezesha wenzake kuanzia safu za ulinzi. Anajua hasa wapi pa kutumia kasi, chenga za mwili kupangua minyororo ya ulinzi. Huyu ndiye Messi tunayemsubiri ndani ya miaka minne ijayo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU