MOROCCO AAHIDI MAKUBWA SINGIDA UNITED

MOROCCO AAHIDI MAKUBWA SINGIDA UNITED

2177
0
KUSHIRIKI

NA SALMA MPELI, ARUSHA


KOCHA mpya wa Singida United, Hemed Morocco, amesema kuwa, moja ya malengo yake ni kuifikisha mbali timu zaidi ya ilipo sasa, katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania msimu ujao.

Morocco alitambulishwa rasmi jana kuvaa viatu vya kocha Hans van der Pluijm, anayekwenda Azam FC, huku kocha huyo msaidizi wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ akipewa kandarasi ya mwaka mmoja.

Akizungumza na BINGWA jijini hapa, baada ya kumalizika kwa mchezo wa fainali ya Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) iliyoikutanisha timu ya Mtibwa na Singida, huku timu yake mpya ikipokea kipigo cha mabao 3-2, Morocco alisema, Singida ina kikosi kizuri, lakini kuna marekebisho kidogo atakayoyafanya.

Alisema, kwa kuwa timu hiyo inakwenda kushiriki mashindano ya SportPesa nchini Kenya, atayatumia kukisoma kikosi chake ili aweze kugundua mapungufu zaidi na kuyafanyia kazi.

“Singida wana kikosi kizuri, lakini katika kizuri chochote hakikosi kasoro, tayari kwa mchezo wao na Mtibwa nimeweza kuona mapungufu machache, lakini nitaweza kuyajua mengi zaidi, kwenye mashindano ya Kenya inapokwenda timu kushiriki,” alisema.

Morocco aliongeza kuwa, mara baada ya kurejea na timu Tanzania, ndipo atakapoanza kazi rasmi ya kufanya maboresho kulingana na mapungufu aliyoyaona, ili kutimiza lengo la kupiga hatua kubwa zaidi ya ilipoishia katika mashindano ya Ligi Kuu msimu ujao.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU