MSIMBAZI WAZUA HOFU KENYA

MSIMBAZI WAZUA HOFU KENYA

6668
0
KUSHIRIKI

NA ALLY KAMWE, NAKURU


ALIYEIMBA wimbo wa ‘Aungurumapo Simba Mcheza Nani’ hakukosea, kwani timu zote zilizotinga hatua ya nusu fainali katika michuano ya SportPesa Super Cup inayoendelea mjini hapa, hazitaki kusikia habari ya kukutana na kikosi cha Simba.

Wekundu wa Msimbazi hao, baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 3-2 dhidi ya Kariobangi Sharks, leo watacheza na Kakamega Home Boys na mashabiki wa Wakenya hao wamejawa na hofu kubwa.

Licha ya kwamba Sharks waliwafunga Yanga mabao 3-1 na kuwatupa nje ya michuano hiyo, mashabiki wao wanayo hofu kubwa kwamba huenda wakakabiliana na kipigo cha ‘mbwa koko’, kutoka kwa Simba, ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hata Kocha Mkuu wa mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Gor Mahia ya Kenya, Dylan Kerr, amesema anaogopa kukutana na Simba kutokana na aina ya kikosi walichonacho.

Akizungumza jana mjini hapa, Kerr, ambaye aliwahi kuifundisha Simba, alisema licha ya kwamba wanacheza na Singida United leo katika mchezo wa hatua hiyo ya nusu fainali, lakini hana hofu kama angeambiwa anakutana na Wekundu wa Msimbazi.

“Simba inao wachezaji wenye uzoefu mkubwa sana, nadhani katika hizi timu ambazo zimeshiriki michuano hii msimu huu wao wanaonekana kuwa wazuri zaidi, nadhani itakuwa kazi kubwa kuwazuia.

“Hawa wanaweza kuwa kikwazo cha sisi kutetea ubingwa wetu kama tutashinda na wao wakashinda kesho (leo), tukakutana fainali, nadhani kuna kazi kubwa ya kufanya, japo bado tunaendelea kuamini kuwa tutafanya vizuri,” alisema.

Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, alisema katika mchezo wa leo dhidi ya Kakamega, hawatataka kwenda mpaka kwenye mikwaju ya penalti kama ilivyotokea mchezo wao wa kwanza na badala yake watamaliza kazi mapema ndani ya dakika 90.

“Mchezo wa kesho (leo) hatutaki tena kwenda kwenye penalti ambazo huwa zinakuwa na presha kubwa na badala yake tunataka kumaliza kazi mapema sana, japo najua utakuwa mchezo mgumu kama ilivyo michezo mingine.

“Kila mmoja anajua kwamba mchezo wetu wa kwanza (dhidi ya Kariobangi), hatukucheza vizuri, lakini tumezungumza na wachezaji, sisi kama benchi la ufundi tunaamini watafanya vizuri zaidi, kwani tumekuja hapa kuhakikisha tunatwaa ubingwa,” alisema.

Bingwa wa michuano hii, mbali ya kupata zawadi, lakini pia atapata bahati ya kwenda England kucheza dhidi ya Everton, inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo na Djuma amesema hilo ndilo lengo lao.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU