MWENZAKO ATAVUTIWA ZAIDI NA WEWE AKIONA WENGINE WANAKUTAFSIRI HIVI

MWENZAKO ATAVUTIWA ZAIDI NA WEWE AKIONA WENGINE WANAKUTAFSIRI HIVI

1070
0
KUSHIRIKI
NA RAMADHANI MASENGA

KUNA tofauti kati ya kuwa hai na kuishi. Kiumbe chochote ambacho hakijafa hicho kiko hai. Kuku yuko hai, ndege, sungura, mateja, wafungwa na hata wagonjwa walio katika vyumba vya wagonjwa mahututi wako hai.

Kuishi ni hali ya kuwa na mamlaka na mazingira unayoishi. Anayeishi vizuri ni yule anayejua nini anafanya, anakimbiza ndoto zake, anamiliki anachotamani na kuishi kwa malengo.

Pia kuna mahusiano yaliyo hai na yale yanayoishi. Mahusiano yaliyo hai ni yale wahusika wanalala tu pamoja, wanakula pamoja na kufanya mambo yao kawaida kila siku. Mahusiano haya mara nyingi hukosa msisimko, raha na burudani.

Kwa sababu hukosa ubunifu, uchangamfu na vitu vipya vya kuchochea hali ya msisimko baina yao. Ili yale mahusiano yanayoishi karibu kila siku huwapa wahusika sababu ya kuona raha na kufurahi.

Kwa sababu wahusika wanajitambua na kujua nini cha kufanya ili kuwepo na raha na msisimko baina yao. Mapenzi ni sanaa. Na hakuna sanaa timilifu ikosayo ufundi. Watu walio katika mahusiano yanayoishi wanatambua dhana hii kwa uhakika kabisa.

Ifahamike bila ujanja, ubunifu na ufundi mahusiano hupoteza msisimko na bashasha. Mwenzako kila siku anaonana na vitu na watu wapya. Watu hao wapya wana sifa na vigezo tofauti.

Kila siku ukiwa yule yule, si mbunifu wala mjanja wa kucheza na akili ya mwenzako basi utafanya akose msisimko kwako na hatimaye kuona yupo yupo tu katika uhusiano na wewe.

Mtu akiwa na fikra hizi basi fahamu uhusiano husika uko katika hali mbaya. Unafanya nini ili mwenzako azidi kubabaika na wewe? Azidi kukuona bora na mwenye kufaa kuliliwa na kupiganiwa?

Kiujumla ya kufanya yako mengi ila hapa nitaeleza machache ambayo kama ukiyafanya kwa makini utafanya mahusiano yako yavutie zaidi huku wewe ukipata thamani na sifa stahiki.

Miongoni mwa mbinu zitakazofanya mwenzako avutiwe zaidi na wewe, ni jamii yako kuvutiwa na wewe. Iko hivi thamani na umuhimu wako kwa mwenzako utazidi kuwa mkubwa ikiwa jamii inayokuzunguka itaonekana ina babaika na wewe katika namna fulani.

Ni mara chache sana binadamu huvutiwa na kitu kinachoepukwa na wengine. Ila silka ya binadamu ni kuvutiwa zaidi na jambo ama kitu kinachoonekana kuvutia wengine.

Ni mara ngapi duka ambalo watu hawapendi kuingia watu wengi wewe unapenda kuingia? Katika mikutano ya siasa watu huvutiwa zaidi na mwanasiasa anayejaza umati mkubwa wa watu kuliko yule anayesikilizwa na watu wachache.

Tafsiri ya kibinadamu huwa mtu anayevutia watu wengi huwa ana kitu bora na thamani zaidi kuliko wengine. Na kwa kuwa ni asili pia ya kibinadamu kupenda kushindana na kufanana basi huwa hataki na yeye kuachwa nyuma. Jamii yako inakutazama vipi?

Ikiwa jamii inayokuzunguka inakuona kama kituko, mtu asiyefaa, wa ovyo basi ni aghalabu sana mwenzako kujihisi fahari kuwa na wewe.

Ili mwenzako ajione wa fahari kuwa na wewe, inabidi jamii inayokuzunguka ikuone bora na wa thamani. Ivutiwe na ichanganyikiwe kwa sababu yako.

Kadiri mwenzako atakavyoona unababaisha mitaa ndivyo atakavyojizatiti kwako. Hakuna mtu mwenye kubabaika na kitu ambacho kina thamani kwake tu ila kwa wengine kinaonekana kama takataka.

Tathmini zinaonesha kuwa watu wenye kukosa thamani kwa wapenzi wao hata mitaani hakuna mtu mwenye kubabaika nao.

Acha kujiweka ovyo. Kuwa mbunifu na wa kisasa. Ukivutia wengine jua utamvutia zaidi mwenzako. Watu wenye kuwababaisha wapenzi wao ni wale wenye kubabaikiwa na jamii ya nje pia.

Kuna watu walikuwa masimulizi ya mtaa kwa namna walivyokuwa wakivutia na kubabaikiwa. Baada ya kuoa ama kuolewa wakajisahau na kuwa wa ovyo. Matokeo yake hata wale walio nao na wao hawaoneshi hali ya kubabaika nao kama ilivyowahi kuwa huko nyuma.

Tambua thamani yako ya mtaani inafanya hata thamani yako ya ndani iwe juu zaidi. Kadiri thamani yako ya nje inavyozidi kuwa kubwa, ndivyo mwenzako naye atakavyozidi kukuthamini na kukujali.

Ili uzidi kufanya mahusiano yako yawe imara na yenye kuvutia inabidi uwe mjanja na utumie akili. Mtaani mwenzako anaona kila aina ya watu.

Anaona wenye kuongea sana, wenye kuvaa vizuri na wenye miondoko ya kila aina. Sasa ili umfanye awe anakufikiria wewe katikati ya hao wote inabidi ucheze na akili yake vilivyo.

Na namna bora ya kucheza na akili yake ni kuona mitaa inavyohangaika juu yako. Kwa sababu hiyo naye atajiona namna alivyobarikiwa kuwa na mtu kama wewe, mtu ambaye anababaikiwa na watu wengi hivyo akili yake itakuwa inakufikiria zaidi wewe kuliko kufikiria hao wengine anaowaona mtaani.

Acha kukaa ilimradi. Tengeneza thamani yako ili mwenzako ajione ana sababu ya kukupigania na kukutunza

 ramadhanimasenga@yahoo.com

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU