MWILI WAKO NI KITU GANI KWA MWENZAKO? JIULIZE HIVI

MWILI WAKO NI KITU GANI KWA MWENZAKO? JIULIZE HIVI

889
0
KUSHIRIKI

NDOA kwa baadhi ya watu inachukuliwa kama sehemu ya kuanzisha familia tu. Baada ya watu wawili kukutana familia inaanza kujengwa kuanzia hapo. Ndiyo, ni sehemu mwafaka kwa ajili ya kujenga familia.

Bila kuwa katika ndoa, tena ndoa imara suala la kujenga familia bora huenda likabaki kuwa ndoto tu. Ila mbali na ukweli huo ni vyema ikatambulika kuwa ndoa ni muunganiko wenye dhamira ya kuleta raha na starehe kwa wahusika.

Katika ndoa kuna amani na furaha ya maisha, kuna furaha na tumaini la kweli. Uwepo wa mtu katika ndoa unatakiwa kuwa na faida ya akili na mwili. Si upo katika ndoa ila amani na tumaini hakuna. Si mtu wa furaha na utulivu stahili, hapana. Haifai kuwa hivyo.

Suala hili linatakiwa kukuletea furaha, amani na uchangamfu. Upate starehe na amani ya kweli katika nafsi yako. Usaliti mwingi katika ndoa unatokea kutokana na wengi kushindwa kuwafanya wenzao kujihisi wa thamani na furaha.

Sikatai, kuwa kuna kundi lipo linafanya usaliti kwa sababu zao binafsi, ila kuna kundi pia linafanywa kufanya usaliti. Na  kuna kundi japo halifanyi usaliti kamili wa kimwili ila linafanya usaliti wa kihisia na kimawazo.

Lipo katika ndoa ila ni kama halipo katika ndoa. Mambo wanayofanyiwa katika uhusiano si ya kuwafanya wawe na amani na furaha. Katika mambo yanayowapa raha wenzao, kwao yamekuwa karaha au fujo zisizo furahisha.

Una hakika mwenzako anafurahia ndoa yenu? Unajua ni kwa kiwango gani mwenzako anaona thamani ya matendo yako kwake? Moja kati ya mambo yanayofanya wengi wasione thamani ya ndoa zao ni kukosa hali ya furaha na amani stahili katika mkutano wa faragha.

Una hakika mpenzi wako anafurahia hali ya makutano yenu faragha? Unafanya vitu gani kufanya mwenzako apate raha na starehe ya faragha?

Mbali na kutakiwa kuwa makini katika mambo mengine ila kubwa angalia kwanza mwili wako. Baada ya kuwa msafi na mwenye kupendeza ila je, mwili wako unakuruhusu kumpa mwenzako starehe stahili?

Wanaume wengi leo wana wake wenye kuona kero kitandani kutokana na ukubwa wa matumbo yao. Wanawake wengi wamekuwa kama mizigo isiyo na tija kwa wenza wao kutokana na ukubwa wa miili yao inayowafanya kuwa kama mizigo wawapo faragha.

Huenda unaona fahari kuwa na mwili mnene ila je, mwili wako hauwi sababu ya mwenzako kukosa anachostahili muwapo faragha?

Katika ukubwa wa kitambi chako je, bado kuna starehe na raha ya mwenzako? Kama kila siku muwapo faragha hakuna raha na starehe anayopata mwenzako unategemea nini?

Ili kila mmoja awe na matamanio ya kukutana na mwenzake kimwili, inabidi kila wakutanapo kila mmoja aondoke akiwa na furaha na kapata raha aliyoitarajia.

Ikiwa kila siku ni wewe unayetoka ukiwa na furaha ila mwenzako hana, jua unauweka uhusiano wako katika hali isiyo ya utulivu hata kidogo. Hata kama hasemi ila jua huenda akafanya au anafanya kitu usichokipenda katika uhusiano wako.

Unene uliokithiri mbali na kukufanya kuwa mvivu uwapo kitandani ila pia unasababisha hata mzunguko wa damu kuwa katika hali isiyo ya kawaida na kusababisha hata viungo vyako vya uzazi kushindwa kufikiwa na damu inavyotakiwa, hali inayopunguza ule msukumo wa kuwa na nguvu uwapo faragha.

Kwa kuwa ni muhimu mwenzako kuwa na furaha na kupata raha muwapo faragha, hakikisha mwili wako unatoa ruhusa ya kufurahia kila kitu mnapokuwa pamoja.

Fanya mazoezi kutengeneza mzunguko mzuri wa damu mwilini pamoja na kuhakikisha mwili wako hauwi sababu ya kumnyima raha mwenzako.

Ukiwa na kitambi kikubwa huwezi kuwa maridadi inavyotakiwa, pia ukiwa na mwili usio umudu pia inakufanya kuwa mzito na kuonekana mzigo kwa mwenzako.

Kweli, wapo wenye miili mikubwa na kuweza kuimudu, hao sina tatizo nao, ila vipi wewe mwenye mwili unaokushinda? Unategemea nini kutoka kwa mwenzako?

Kila siku uwe ni wewe tu unayetoka ukiwa na furaha ila mwenzako ni majonzi. Mpaka lini hali hiyo? Kuwa makini! Jifanye kuwa starehe na raha ya mwenzako ili ndoa yako iwe ya amani na starehe.

ramadhanimasenga@yahoo.com

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU