PIERRE: HII NI TRELA, SUBIRINI PICHA KAMILI

PIERRE: HII NI TRELA, SUBIRINI PICHA KAMILI

1456
0
KUSHIRIKI

NA CLARA ALPHONCE, SINGIDA


 

BAADA ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Simba, Pierre Lechantre, amewaahidi mashabiki wa klabu hiyo kushuhudia kikosi chao kikiwa katika ubora wa hali ya juu msimu ujao kutokana na ‘nondo’ za uhakika atakazowapa vijana wake.

Pamoja na kuipa ubingwa Simba, Pierre ametamba kuwa bado hajatoa ujuzi wake wote alionao kwani kwa muda aliokuwapo Msimbazi, alikuwa akiwasoma wachezaji, viongozi, mashabiki, mfumo wa ligi na klabu hiyo kwa ujumla.

Akizungumza na BINGWA mjini hapa juzi, Kocha huyo raia wa Ufaransa alisema alipofika Simba, alipewa kazi mbili ambazo zote amefauli; ya kwanza ikiwa ni kuipa ubingwa timu hiyo na ya pili kuifunga Yanga.

Alisema hata ufundi aliokuwa akiutoa, haukuwa ukilenga kusuka kikosi cha ‘maangamizi’, bali alilenga kutwaa ubingwa kama alivyokubaliana na uongozi wa klabu hiyo.

Alisema kwa kuwa aliikuta timu tayari ipo kwenye mashindano, hakuwa na kazi nyingine zaidi ya kuhakikisha inapata ushindi bila kujali idadi ya mabao waliyokuwa wakishinda.

“Kwa sasa mkataba wangu umemalizika, kazi waliyonipa nimemaliza, hivyo kama tukifikia makubaliano ya mkataba mpya, kazi kubwa itakuwa kuijenga timu itakayokuwa ikicheza mpira wa pasi na kufunga idadi kubwa ya mabao msimu ujao.

“Nafahamu baada ya ubingwa, Simba wanahitaji kuona timu yao inafanya vizuri katika michuano ya kimataifa, hivyo tutafanya usajili mzuri kuboresha kikosi changu ili kiwe katika ubora wa hali ya juu na kuwa tayari kutoa upinzani dhidi ya timu kubwa Afrika,” alisema Pierre.

Katika hatua nyingine, Meneja wa Simba, Richard Robert, amesema wanatarajia kufanya sherehe kubwa ya ubingwa mara baada ya kumalizika kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Simba ilijihakikishia ubingwa rasmi katikati ya wiki iliyopita baada ya Yanga waliokuwa wapinzani wao katika mbio hizo, walipofungwa na Prisons ya Mbeya mabao 2-0, kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Pamoja na hilo, bado Wekundu wa Msimbazi hao hawakutaka kuwa na huruma mbele ya Singida United waliovaana nao juzi Jumamosi na kuwachapa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Namfua, Singida, hivyo kufikisha pointi 78 kutokana na mechi 28.

Msafara wa Simba leo unatarajiwa kutembelea bungeni mjini Dodoma walikoalikwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai pamoja na wabunge ambao ni wapenzi wa timu hiyo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU