SHUKRANI: POGBA MCHEZAJI BORA APRILI, AMSHUKURU MOURINHO

SHUKRANI: POGBA MCHEZAJI BORA APRILI, AMSHUKURU MOURINHO

8263
0
KUSHIRIKI

 

MANCHESTER, England


 

 

KIUNGO wa klabu ya Manchester United, Paul Pogba, ametanguliza shukrani kwa kocha wake, Jose Mourinho, kwa kitendo cha kumwamini baada ya kukabidhiwa tuzo ya Mchezaji Bora Aprili.

Mfaransa huyo alifanikiwa kunyakua tuzo hiyo ya pili kwa msimu huu akiwashinda nyota kama Ander Herrera na Alexis Sanchez ambao anacheza nao pamoja United, baada ya kupita miezi saba tangu alipotwaa ya kwanza.

Katika miezi michache tangu mwaka huu uanze, Pogba hakuwa na wakati mzuri. Kiungo huyo alitibuana na Mourinho na kujikuta akiachwa na kikosi kutokana na kiwango kibovu alichokuwa akikionesha katika mechi kadhaa.

Lakini, katika kipindi cha hivi karibuni, mchezaji huyo amebadilika na kurudi kwenye kiwango chake, akiweza kufunga mabao matatu na kutoa pasi mbili za mabao katika mechi alizopangwa na Mourinho.

“Ni jambo jema kama unafanya kazi na kocha anayekuamini wewe na wenzako. Ningependa kuwashukuru wote walionipigia kura ili nishinde tuzo hii,” alisema Pogba.

Maelewano hafifu baina ya Mourinho na Pogba yalianza kuonekana baada ya kocha huyo kumfanyia mabadiliko kiungo wake huyo katika mtanange dhidi ya Bournemouth, mapema Aprili.

Hata hivyo, Pogba katika mechi kadhaa zilizopita, alionesha mabadiliko makubwa katika uchezaji wake na kuzima maneno kuwa yeye na Mourinho haziivi.

Kiungo huyo alisisitiza kwamba, kwa sasa akili yake imeegemea katika suala la kuisaidia klabu itimize malengo yake msimu huu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU