SIMBA RED LION: NYIE CHONGENI TU, SISI TUNAHESABU POINTI TATU

SIMBA RED LION: NYIE CHONGENI TU, SISI TUNAHESABU POINTI TATU

1096
0
KUSHIRIKI

NA MARTIN MAZUGWA

KARIBU msomaji wa safu hii ya Tawi kwa Tawi inayokujia kila Jumamosi, ambapo leo tumetembelea moja kati ya matawi makongwe ya klabu ya Simba, linalofahamika kama Red Lion lenye maskani yake Kawe, jijini Dar es Salaam.

Tawi hilo ambalo lilianzishwa Februari 28, 1992 likiwa na wanachama 10 pekee wenye kadi za timu hiyo, huku wengine zaidi ya 15 wakiwa kama mashabiki wa kawaida.

Lengo la kuanzishwa tawi hilo lilikuwa ni kuongeza idadi ya wanachama ndani ya klabu hiyo ambao watasaidia timu kwa michango mbalimbali ili kuhakikisha inafanya vizuri hususan katika michuano ya kimataifa.

Hivi sasa tawi hilo lina wanachama zaidi ya 50 wenye kadi halali za klabu ambao wamekuwa wakijitolea kwa hali na mali kuhakikisha timu inafanya vizuri na kubeba taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara walilolikosa kwa misimu zaidi ya mitatu.

BINGWA lilitembelea tawi hilo na kufanya mazungumzo na Katibu mkuu wa tawi hilo, Abdul Malufu, ambaye alisema kuwa malengo yao msimu huu ni kubeba taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ambalo hawajalibeba kwa misimu minne.

Alisema kuwa huu ni msimu wao, wamechoshwa na kebehi zinazotolewa na watani wao wa jadi ambao wamekuwa wakiwapa majina ya ajabu ajabu, hivyo msimu huu wameamua kufanya vizuri ili kuwaziba midomo.

Malufu alisema kuwa mipango waliyopanga msimu huu ni kuhakikisha timu yao kushinda kila mchezo ili kurudisha heshima ambayo ilianza kupotea kutokana na matokeo yasiyoridhisha.

Tuna imani kocha mkuu Joseph Omog ni kati ya walimu bora katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, kwani ni kocha wa kwanza kuipa timu ya Azam taji.

Alisema mwalimu amejitahidi sana kukifanyia marekebisho kikosi, tunaimani naye atafanya makubwa na kutupatia taji na kuweka historia katika klabu yetu kama alivyofanya kwa Azam FC.

Tumekaa kipindi kirefu bila kutwaa taji, ni muda wetu misimu iliyopita tulikuwa hatufanyi vizuri kutokana na migogoro iliyokuwapo klabuni, lakini pia ufinyu wa kikosi lakini hivi sasa hali ya kikosi chetu ni nzuri tunao wachezaji wengi na wenye uwezo mkubwa wa kubadilisha matokeo wakati wowote.

Ukiangalia msimu uliopita tulikuwa tukiwategemea zaidi Hamis Kiiza na Ibrahim Ajib, ambao kama mchezo ukiwa mgumu tulikuwa tukipoteza kirahisi sana lakini angalia hivi sasa tuna Pastory Athanas, Juma Liuzio, Mohamed Ibrahim, Laudit Mavugo kikosi kimetimia wapinzani wakae mkao wa kupokea kichapo tu hatutaki masikhara msimu huu.

Mtani wetu ajiandae kipigo mzunguko wa pili maandalizi tuliyoyafanya si ya mchezo na tutahakikisha tunaziba mianya yote ya hujuma kwani mchezo uliopita mwamuzi hakututendea haki, lakini mzunguko huu hatutakubali ujinga ule ujirudie tena.

Mzunguko huu hatoki salama, kwani tutahakikisha tunaweka ulinzi wa kutosha uwanjani ili wasiweze kucheza mpira nje ya uwanja kama kawaida yao.

Matawi yote ya klabu ya Simba tunatakiwa kuungana na kuwa kitu kimoja ili tuweze kurudisha ufalme wetu ambao ulianza kupotea kutokana na migogoro ambayo haikuwa na msingi tunamshukuru Rais wa timu Evans Aveva, kwa kuimarisha umoja miongoni mwetu.

Huu ni muda wa ‘Mnyama’ kurudisha heshima, waache waendelee kupiga domo kuwa tunashinda ushindi mwembamba lakini tunaendelea kuhesabu pointi tatu kila mchezo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU