TAFSIRI YA KISASI KATIKA MAPENZI

TAFSIRI YA KISASI KATIKA MAPENZI

902
0
KUSHIRIKI

KUNA watu wanaumizwa katika mapenzi. Kuna watu wana furaha sana katika mapenzi. Tathmini inaonesha anayeishi na furaha katika mahusiano yake hutawaliwa na amani muda mwingi katika maisha yake hata kama kuna baadhi ya mipango ama mambo katika maisha yake hayako sawa.

Halikadhalika imethibitika kuwa mwenye kuishi katika uhusiano usio na amani, uliojaa huzuni na karaha, anakuwa katawaliwa na huzuni na majonzi muda mwingi katika maisha yake hata kama kuna mipango ama mambo yake mengine ya kimaisha yako sawa.

Kumefanyika tathmini ya watendaji katika maofisi mengi. Tathmini inaonesha wale ambao wanaenda kazini huku wakiwa na msongo wa mawazo unaotokana na mahusiano yao, hata utendaji kazi wao huwa si mzuri.

Hujikuta hawana amani kukaa ofisini na wala hawatamani kukaa nyumbani. Kwa ajili hiyo, wanajikuta muda mwingi wakiwa wamejiinamia katika meza zao ama sehemu zao za kazi bila kujua wanachofanya.

Pia mtu mwenye uhusiano mzuri, wenye amani na raha, huwa mchangamfu si tu mbele ya marafiki zake bali hata kazini. Kutokana na uchangamfu huo, hufanya hata utendaji wake wa kazi uwe juu zaidi.

Maana ya kusema hayo ni kwamba, mahusiano ya kimapenzi ni sehemu muhimu mno katika maisha yetu. Si sehemu tu ya kutimiza ratiba ila ni sehemu yenye mchango mkubwa sana katika ustawi wako wa furaha amani na hata maendeleo yako ya kimaisha.

Sisi wataalamu wa masuala ya saikolojia ya mapenzi tuna amini matatizo mengi ya kiakili yanasababishwa na watu wengi kuzama katika misongo ya mawazo inayotokana na mapenzi.

Kama suala la mapenzi kwa mtu likiwa haliko sawa basi hata baraka zake alizopewa na Mungu, mhusika anaweza kutoziangalia kwa jicho bora na la kushukuru zaidi.

Tumeshuhudia mara nyingi matajiri wakilia kutokana na mapenzi. Tumeona mara nyingi vijana watanashati, wasomi na wenye mafanikio wakijiua kutokana na masuala ya mapenzi.

Pumziko la mapenzi linampa mtu faraja, raha na pumbazo muhimu linalomfanya aone maisha ni kitu bora na mwafaka sana.

Pia machafuko ya kimapenzi yanamfanya mtu ajione hana hadhi maana ana sababu ya kufurahia maisha yake. Siku kadhaa nyuma nilimsikia mtu akisema anatamani kumlipizia kisasi mpenzi wake.

Alisema kwa miezi kadhaa ya kuwa naye katika mahusiano, alikuwa akimfanyia mambo mengi mazuri. Alikuwa akimpa pesa, zawadi na muda wake mwingi.

Ila pamoja na hayo yote (mazuri) alikuja kugundua bado mpenzi wake anawasiliana na mpenzi wake wa zamani. Kwa kufanya hivyo, jamaa anasema aliona hana thamani tena kwa mpenzi wake hivyo aliamua kumuacha na kutaka kumlipizia kisasi.

Kwanza nilishangaa kusikia hivyo. kuwasiliana na mpenzi wa zamani, tafsiri yake haitakiwi moja kwa moja kuwa anampenda. Kuna mambo mengi yanayoweza kumsukuma mtu kufanya hivyo. Nitayaeleza kwa ufupi.

Kwanza kuachana tafsiri yake si uadui. Kuachana maana yake ni kwamba wamepimana na kuona katika suala la mapenzi wenyewe hawaendani.

Huenda ni kutokana na tabia na misimamo yao ama wamegundua kuwa waliingia katika mapenzi kutokana na hamasa tu ila hawana hisia za dhati juu ya mapenzi. Kutokana na sababu hizo wanaweza kuachana na kubaki tu wakiwasiliana katika mambo mengine.

Japo mawasiliano haya hayafai na haipendezi kuyafanya mara kwa mara.

Ila pia, hata kama wanawasiliana katika namna ya kimapenzi. Unadhani kosa ni lake moja kwa moja? Hapana.

Kosa hapo si lake moja kwa moja. Huenda wanawasiliana na ex wake kwa sababu kuna mambo wewe bado hujaweza kufanya kwake katika hali bora hivyo kushindwa kufuta kumbukumbu za mpenzi wake wa zamani katika hisia na akili yake.

Tafakari hili. Kakaa naye katika uhusiano kwa zaidi ya miezi tisa ama kumi. Hapo wamefanya na kuongea mengi. Wamepitia katika vipindi tofauti vya maisha kisha baadaye wakaachana baada ya kuona hawaendani.

Wewe ndani ya miezi yako mitatu toka muwe pamoja, unadhani jukumu lako ni kumpa pesa na kulala naye kitanda kimoja tu.

Toka awe na wewe bado anahisi kuna mambo mengi unatakiwa kumfanyia ila humfanyii. Katika namna hii, katika hali ya kibinadamu hujikuta akiwasiliana na mhusika.

Anawasiliana naye kwa sababu kuna harufu fulani nzuri bado inanukia upande ule na kwako bado hupulizi harufu nzuri zaidi ya kuifanya pua yake isinuse sehemu nyingine.

Iko hivi. Inauma sana mpenzi wako kuwasiliana na mpenzi wake wa zamani ambaye aliamua kuachana naye. Ila hii haiondoi ukweli kwamba kitu kizuri daima huwa kinakumbukwa.

Ili mwenzako aachane na kufikiria ya mpenzi wake wa zamani, amua kuwa bora na mahiri zaidi. Kuwa mbunifu na mwenye kujua shida zake za kihisia na kuzitatua kwa ubunifu na weledi.

Kwa kufanya hivi kwa kipindi kirefu, atajikuta akiona kwako ni mahala bora zaidi na kujipongeza kuachana na yule wa zamani na kuwa na wewe.

Ila pia tafsiri ya kisasi katika uhusiano ni kwamba, mhusika anataka kumfanyia fulani kisasi kwa sababu bado anamfikiria, anamuhisi katika hisia zake na anaumia kwa kuwa naye mbali.

Kwa lugha moja ni kwamba, bado anampenda sana. Upendo huu ndiyo unamfanya aumie hivyo kutamani kumuumiza mwenzake ili wachangie maumivu.

Sasa kama bado unampenda, kwanini usifanye mipango ya kuwa naye tena badala ya kuumiza kichwa kuwaza namna ya kumfanyia kitu ambacho unakitafsiri kama kisasi?

Kama umeamua kuachana naye kwa dhati, basi kisasi bora cha kumfanyia mwenzako, ni kuwa na mtu mwingine unayependana naye kisha ukaamua kumfanyia mtu huyo matendo mazuri sana.

Matendo yatakayomfanya aimbe sifa zako kila mahali hata ex wako akazisikia na kujikuta akijutia kuachana na wewe. Hicho ni kisasi bora zaidi. Kinyume na hapo hakuna maana ya kulipiza kisasi.

Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia( Psychoanalyst)

ramadhanimasenga@yahoo.com

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU