TETEMEKO BUNGENI,NI BAADA YA KIKOSI CHA SIMBA KUTIA TIMU,OKWI KAMA MFALME, WABUNGE...

TETEMEKO BUNGENI,NI BAADA YA KIKOSI CHA SIMBA KUTIA TIMU,OKWI KAMA MFALME, WABUNGE WA YANGA WAWEWESEKA

7734
0
KUSHIRIKI

NA RAMADHAN HASSAN, DODOMA


 

*Ni baada ya kikosi cha Simba kutia timu

* Okwi kama mfalme, wabunge wa Yanga waweweseka

UKUMBI wa Bunge mjini Dodoma, ulitetemeka jana kutokana na nderemo, vifijo na shangwe baada ya msafara wa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba kuingia.

Mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga, alitangaza uwepo wa timu hiyo na kuamsha shangwe kutoka kwa wabunge wa Simba.

“Tuna wageni wa Mheshimiwa Spika ambao ni viongozi 10 na wachezaji 48 wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambao ni Simba SC,” alisema Giga.

Baada ya taarifa hiyo, baadhi ya wabunge ambao ni mashabiki wa Simba walisimama na kuanza kupiga makofi yaliyoambatana na shangwe.

Miongoni mwa wabunge waliodhihirisha unazi wao ni Mbunge wa Lushoto, Shaban Shekilindi (CCM) ambaye alisimama akiwa na jezi ya klabu hiyo iliyokuwa na maandishi ‘Simba Bingwa 2018-2019’.

“Waheshimiwa wabunge naomba tusikilizane, naamini kabisa vifijo hivi vimesaidiwa na wabunge, mashabiki wa Yanga kwa vile ni waungwana,” alisema Giga huku wabunge wakizidi kushangilia wakisema ‘This is Simba’.

Mwenyekiti huyo alisema timu hiyo ilikuwa imeongozana na Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, mwanachama na mfanyabiashara wa timu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’, Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage na Msemaji wao, Haji Manara.

“Waheshimiwa wabunge, pia tuna ndugu Emmanuel Okwi, huyu kwa sasa ndiye mfungaji bora na ndiye Balozi wa Mbeya Tulia Ackson Marathon.

“Waheshimiwa wabunge, tunajua kabisa Yanga ni timu ambayo wenzetu hawa ni waungwana wazuri sana,” alisema huku wabunge wakishangilia.

Awali, wakati akijibu maswali, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda, alisema anaamini Simba itatumia vizuri fursa ya kushiriki michuano ya kimataifa.

“Naamini Watanzania watapata wawakilishi kwenye michezo ya kimataifa ambao hawatatupa presha, kwa sababu vijana hawa wanajua kuucheza vizuri sana mpira wa miguu,” alisema.

Mbunge wa Ilala, Musa Zungu (CCM), wakati akiuliza swali alipiga kijembe baada ya kusema: “Humu ndani ameingia mnyama mkali, lakini tupo salama.”

Naye Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, kabla ya kujibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mwantumu Dau Haji (CCM), alinogesha kijembe cha Zungu kwa  methali isemayo  kwa kusema, ‘Mla kala leo mla jana kala nini?’

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Kangi Lugola, alisema matamko kama ya Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara yanaruhusiwa.

“Watu walipiga makele sana nikaulizwa haya makelele kwa mujibu wa mazingira yana mahusiano gani, nikasema kwa mujibu wa kifungu cha 106 makelele yanazuiliwa, lakini yale ya kushabikia kama matamko ya Haji Manara yanaruhusiwa,” alisema na kushangiliwa na baadhi ya wabunge.

Mara baada ya wachezaji na viongozi kutoka nje ya Bunge, wabunge na wafanyakazi wa Bunge walipata fursa ya kupiga picha na wachezaji, lakini kivutio alikuwa Okwi ambaye wengi wao walimkimbilia.

Simba ilitinga bungeni ikitokea Singida, Jumamosi ilicheza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida United na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU