UDAMBWIDAMBWI WA MARCELO

UDAMBWIDAMBWI WA MARCELO

1489
0
KUSHIRIKI

Na MARKUS MPANGALA

JINA lake ni Marcelo Vieira da Silva Junior. Tamka Machelo. Anavaa jezi namba 12 mgongoni. Ni Mbrazil aliyerithi beki tatu kutoka kwa Roberto Carlos.

Kabla ya Zinedine Zidane kubadilisha mbinu za kumtumia Cristiano Ronaldo kutoka winga ya kushoto au kulia hadi mshambuliaji wa kati, kuna jambo moja ambalo linatokea kila siku.

Kama Ronaldo akipangwa winga ya kushoto basi kazi ilikuwa rahisi kwakuwa Marcelo alikuwa na uwezo wa kupanda mno hadi eneo la boksi la adui.

Unaposhambulia timu pinzani ukitaka kupitia kushoto basi peleka pasi kwa Marcelo. Ni Marcelo anajua tuanzie kushoto kuingia katikati ya dimba tukielekea kwenye 18 au tushambulie kushoto moja kwa moja. Kama anaingia katikati ya dimba kuelekea kwenye 18 maana yake anakokota mwenyewe huo mpira kabla ya kugawa kwa wafungaji.

Na kama anakokota kwenda upande wa kushoto maana yake anazifuata nyendo za Ronaldo. Naye anaweza kupokea pasi na kuirudisha kisha anatafuta upenyo wa kuingia eneo la hatari, kabla hajapishana na Karim Benzema ili kutenga nafasi ya kupachika bao.

Chukulia mfano wakati Javi Martinez alipomfanyia faulo Ronaldo kwenye pambano la kwanza la ligi ya mabingwa pale Allianz Arena, jijini Munich, Ujerumani.

Kimsingi Ronaldo alifanya kazi ya kumtafutia kadi Martinez, kama ambavyo Marco Asensio alivyomfanyi Vidal. Pasi hiyo ilitoka kwa Marcelo ambaye alikuwa upande wa kushoto nje ya 18, akampasia Ronaldo aliyekuwa akiingia kwenye boksi la Bayern Munich.

Matokeo yake Martinez akamvaa Ronaldo mzima mzima, ikawa faulo. Kisha akatolewa nje kwa kadi ya pili ya njano. Kulikuwa na uzembe fulani kwa Martinez. Na hivyo hivyo kwa Vidal.

Katika kikosi cha Real Madrid kuna wachezaji wawili ni wakali wa kutuliza mpira, iwe kifuani, gotini au miguuni. Ni Marcelo na Karim Benzema. Wawili hawa wakipigiwa pasi ya aina yoyote wana wepesi fulani ya kunasa au kuituliza mipira kwa namna yao.

Tukirudi kwenye mbinu za Zidane kumbadilisha Ronaldo, iko hivi. Kwa sasa Ronaldo hana ile kasi kama zamani. Hawezi kukimbiza mabeki kama zamani. Hawezi kuwa na kasi kama zamani. Wala ile akili ya kupigania tuzo binafsi hana. Zidane amepunguza ile hali ya Ronaldo kujipigania zaidi pamoja na timu kutegemea mabega yake kubeba mizigo yote ya ushindi.

Zinedine Zidane anaamini Ronaldo bado anao uwezo. Nami ninaamini kuwa Ronaldo bado anao uwezo wa kupachika mabao katika mechi yoyote. Ana umri wa miaka 32 kwa sasa. Ameingizwa kwenye kikosi cha Madrid kama mshambuliaji wa kati.

Nafasi hii imemfanya Karim Benzema acheze kwenye eneo dogo zaidi. Ronaldo amepewa uhuru kwenye nafasi ya nambari 9 kiasi kwamba amekuwa akimnyima nafasi Karim.

Hii ni kwamba, Karim Benzema analazimika kupisha eneo la mshambuliaji wa kati ili kumwachia nafasi Ronaldo. Mabao yote aliyofunga si kama yale ya kukimbizana na mabeki.

Badala yake mabao yote amefunga akiwa kwenye boksi la adui. Kazi yake akiwa namba 9 ni kumalizia pasi za mwisho. Anapachika mabao tu. Ronaldo wa sasa hafanyi kazi kubwa kama zamani ya kukimbizana na mabeki kutoka nusu ya uwanja hadi lango la adui.

Kwenye pambano la marudiano la juzi dhidi ya Bayern Munich, nafasi ya Ronaldo imejidhihirisha zaidi. Mabadiliko ya kumtoa Karim Benzema na nafasi yake kuchukuliwa na Marco Asensio maana yake Ronaldo alikuwa ameachwa peke yake pale mbele.

Sasa ilikuwa Ronaldo anacheza peke yake kama nambari 9 kuliko kupishana na Karim Benzema. Likaja kosa jingine kwa Bayern Munich, kutolewa kwa kadi ya pili ya njano kwa Arturo Vidal.

Mimi naamini ulikuwa uzembe mkubwa kwa Vidal. Alitafutiwa kadi naye akajizamisha kirahisi mno kwa kupandisha mguu wa kushoto uliomchota Marco Asensio, huku tayari wa kulia ukiwa umefanya faulo ambayo ingeachwa kirahisi.

Wakati mabadiliko hayo yalipofanyika kwa Bayern kutoka Alonso, upesi Zinedine Zidane alikuwa anazungumza na Marcelo pembeni mwa uwanja. Walizungumza na kuelezana. Nilisubiri nini kitatokea kwa Marcelo.

Nilichoshuhudia ni ufundi wa hali ya juu. Ndiyo ukawa sababu ya bao la tatu la Ronaldo. Lakini nakufikirisha msomaji wangu rudisha kumbukumbu Marcelo alitoka wapi na ule mpira hadi kuingia eneo la hatari la Bayern Munich? Wakati akifanya yote hayo wachezaji wa Bayern Munich walikuwa wapi na kwanini hawakumzuia?

Nini tafsiri ya upatikanaji wa lile bao? Tayari kocha alishamtoa Toni Kroos na Isco. Maana yake eneo la kiungo lilikuwa mali ya Luka Modric na Casemiro. Wawili hao ndio walikuwa akizunguka katikati.

Marcelo baada ya kuzungumza na Zidane alibadilika na kuingia zaidi eneo la katikati ya dimba ikiwa na maana ya kumrudisha nyuma Thiago Alcantara. Marcelo alikuwa kiungo msaidizi na matunda yake yalikuwa bao la Ronaldo.

Marcelo alipokea pasi katikati ya uwanja, tena akiwa eneo la Madrid, alikimbia nusu ya uwanja na kuwalamba chenga mmoja na mwingine. Alipokaribia eneo la 18 Marcelo alikuwa amekumbana na wachezaji 6 wa Bayern, lakini wote akawapita kabla ya kumpa pande Ronaldo. Marcelo aliwanyanyasa, akawaonyesha udambwidambwi alivyopenda. Halafu akampa pasi Kingnaldo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU