ULITAKA LUKAKU AFANYE NINI ZAIDI?

ULITAKA LUKAKU AFANYE NINI ZAIDI?

1006
0
KUSHIRIKI

NA OSCAR OSCAR

ASIKWAMBIE mtu kitu, Manchester United si klabu ya kawaida nchini England na hata barani Ulaya. Huwezi kutaja klabu za soka tajiri duniani ukaiacha Manchester United. Huwezi kutaja klabu zenye mashabiki wengi duniani ukaiacha Manchester United.

Hii ni aina ya klabu ambayo wachezaji wengi duniani hutaka kutimiza ndoto zao kwa kucheza hapo. Endapo utakuwa umesahau, Manchester United ndiyo klabu yenye mafanikio zaidi England.

Unaanzaje kuikataa klabu ya mtindo? Asikwambie mtu, hakuna mchezaji ndani ya England anayeweza kuikataa Manchester United, labda awe anatoka Liverpool. Asikwambie mtu kitu, hakuna mchezaji anayetoka Chelsea, Arsenal anayeweza kuikataa ofa nono kutoka Manchester United. Sembuse Everton?

Hapana, hakukuwa na namna kwa Romelu Lukaku. Everton ni klabu ilyomkuza sana Lukaku, lakini haina uhakika wa kushinda taji lolote hivi karibuni. Huwezi kuwa mchezaji bora duniani bila kuwa na ndoto za kushinda mataji makubwa duniani. Everton ni klabu kubwa na yenye historia kubwa England, lakini kwa sasa huwezi tena kumfanya atimize ndoto zake.

Ni kweli Everton ndiyo klabu iliyoshiriki mara nyingi zaidi misimu ya Ligi Kuu nchini England kuliko nyingine yoyote. Wameshiriki katika misimu 114. Hakuna klabu yoyote inayowagusa lakini hiki si kigezo cha kumbakisha Lukaku.

Ni kweli Everton ni mabingwa mara tisa wa EPL, mara tatu zaidi ya Chelsea lakini hata hii si sifa ya kumbakisha Lukaku. Baada ya kuondoka kwa Wayne Rooney na Zlatan Ibrahimovic kuondoka ndani ya Manchester United, kunaacha nafasi huru sana kwa Lukaku kutakata ndani ya Old Trafford.

Mshindani pekee kwenye nafasi ya ushambuliaji pale Old Tafford ni Markus Rashford, ambaye msimu uliopita hakufikia hata nusu ya magoli ya Lukaku kwenye EPL.

Unapohitaji kuwa mchezaji mkubwa duniani ni lazima ucheze kwenye timu kubwa. Ulitaka Lukaku afanye nini tofauti na kusaini Manchester United? Hakuna. Pamoja na Jose Mourinho kutompa nafasi kipindi wote wawili wako Darajani, lakini haina ubishi kwamba, Romelu Lukaku kwa sasa ni moja kati ya washambuliaji hodari sana nchini England.

Ni kweli klabu ya zamani ya Lukaku, Chelsea walimhitaji zaidi mchezaji huyola lakini kuikataa ofa ya Manchester United si jambo rahisi. United wamejipambanua kama moja ya klabu bora sana Ulaya. Ni aina ya klabu kama Bayern Munich, Barcelona na Real Madrid. Nadra sana mchezaji kukataa ofa yao. Old Trafford ni sehemu inayohitaji mfalme mpya.

Si rahisi sana kwa Lukaku lakini kwa kuangalia umri wake na ubora, Lukaku ana nafasi kubwa ya kuandika jina lake ndani ya mioyo ya mashabiki wa United. Katika misimu mitano ya Lukaku ndani ya Ligi Kuu nchini England, hakuna msimu hata mmoja aliofunga chini ya goli 10. Ni aina ya mchezaji ambaye anakupa uhakika wa kuanzia goli 15 kila msimu. Ni aina ya mchezaji ambaye bado anaweza kucheza soka hata kwa misimu 10 ijayo. Haikuwa rahisi kwa Lukaku kutanba pale Stamford bridge kwa sababu Chelsea ilikuwa na wafalme wengi wanaocheza kwenye nafsi ya ushambuliaji.

Alikuwapo Didier Drogba, alikuwapo Fernando Torres. Ungemweka wapi Lukaku? Hakukuwa na nafsi yake. Zama zinabadilika, ile ya Manchester United ya kina Carlos Tevez, Dimidtry Babertov, Cristiano Ronaldo na Wayne Rooney haipo tena. Ni wakati wa kumsaka mfalme mpya wa Old Trafford. Anawaza kuwa Paul Pogba, anaweza kuwa Eric Baily au hata Lukaku huwezi jua.

Mourinho amekuwa muumini mkubwa sana wa wachezaji wasio na mambo mengi mbele ya lango, Lukaku ni miongoni mwa wachezaji wa aina hiyo. Hajui kuremba, anajua kutupia tu. Mguu wake wa dhahabu umekuwa ukimfanya kila wakati akimbie kwenye kibendera kwenda kushangilia. Magoli 25 aliyofunga msimu uliopita akiwa na Everton yanathibitisha uwezo huo.

Manchester United haina mfalme kwa sasa, kazi kwake kuandikisha historia mpya. Anaondoka Everton kama shujaa baada ya kuweka rekodi ya kuwa moja ya wachezaji watano kuwahi kufunga magoli 50 kabla ya kutimiza miaka 23, lakini ana mlima mrefu wa kuandika historia nyingine ndani ya Old Trafford.

Mjadala unaweza kujikita zaidi kwenye kiasi kikubwa cha fedha kilichotumika kumnasa Lukaku, lakini kuhusu uwezo, hakuna shaka anakwenda kuibeba United kuelekea msimu ujao, kazi yake kubwa ni kufunga magoli na hakika hajawahi kuishindwa. Manchester United inahitaji mfalme mpya kwa sasa, kama si Lukaku basi anaweza kuwa Paul Pogba.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU