UNAWEKEZA NINI KATIKA HISIA ZA MWENZAKO? FANYA HIVI

UNAWEKEZA NINI KATIKA HISIA ZA MWENZAKO? FANYA HIVI

744
0
KUSHIRIKI

 

KILA tendo ama tukio kwa mwenzako linampa tafsiri fulani juu ya tabia yako ama namna unavyomchukulia. Kama matendo yako kwake ni mazuri na yenye kutia faraja, atakuona ni mtu bora na mwenye maana.

Kwa kuwaza hivi, atajiachia kwako na kufanya matendo mema ili akutunze na asikupotee. Ila ikiwa matendo yako ni ya ovyo, yanakera na kuumiza basi mwenzako atakuchukulia kama mtu mjinga, usiyejali na mwenye kufaa kuepukwa.

Hata kama hawezi kukuepuka leo labda kutokana na upendo mkubwa alionao juu yako, ila jua ipo siku tu atakuacha solemba na kutafuta anayemwona anamfaa katika maisha yake.

Mwenzako akihisi na kuamini kwa dhati kwamba wewe si mtu mwenye kumfaa kutokana na matendo yako, mchakato wa kukuacha huanza mara moja.

Jambo la kwanza kulifanya ili aweze kujiengua katika maisha yako, ni kuanza kutokufikiria katika maisha yake ya baadaye. Ijulikane watu wowote wanaopendana na kuaminiana huwa wanafikiriana katika maisha yao ya baadaye.

Katika kufikiriana huku katika maisha ya baadaye ndipo mtu akiachwa ghafla huwa akichanganyikiwa kwa sababu anakuwa kakatishwa katika ndoto yake tamu ya kimapenzi.

Swali, unawekeza kitu gani katika hisia za mwenzako? Matendo yako kwa mwenzako yakoje? Matendo yako kwa mwenzako yanamfanya akufikirie vipi?

Kila tukio lako kwa mwenzako linabeba hatima ya maisha yao. Uonapo watu wanapendana na kuaminiana sana leo, jua mzizi wa upendo huo umejengwa jana. Hata ukiona watu wanaachana jua mbegu ya utengano wao haikuanza leo.

Hata kama mwenzako anakupenda sana, anakujali sana na una amini hawezi kukuacha ila jua mfululizo wa matendo yako ya ovyo kwake yatayeyusha upendo wake na kumfanya aanze kukufikiria kama mtu wa ovyo.

Mapenzi ili yawe imara inabidi ufanye uwekezaji mkubwa sana katika maisha ya mwenzako. Hakikisha kila tendo lako linaacha kumbukumbu nzuri na ya kusisimua.

Usione watu wakiwa wanapendwa sana na ukadhani hayo yametokea bahati mbaya. Hapana. Kuna watu wanajua namna ya kucheza na hisia na akili za wenzako.

Kila jambo wenzao wanalotamani kufanyiwa wao wanalifanya. Kila wenzao wanapokuwa na huzuni na msongo wa mawazo wao wanajua namna ya kuwachangamsha na kuwafanya wapate upya sababu ya kufurahia maisha.

Fahamu uchawi wa kwanza unaoweza kumroga mwenzako ni kujua namna ya kucheza na hisia zake. Kama ukiwa na ufahamu wa kutosha namna ya kumfanya afurahi sana ama ahuzunike kisha ukachagua kumfanya afurahi na achanganyikiwe kwa ajili yako basi uchawi huu ni mkubwa na utamfanya akuwaze na kutukuza jina lako mara zote.

Usiyafanye maisha yako ya uhusiano kama marudio ya matendo yako ya kila siku. Kwa kuyafanya hivyo jua mapenzi yako yanakosa msisimko stahili.

Hutapendwa kwa kusema naomba unipende. Hutapendwa kwa kumlilia sana mpenzi wako. Ila utapendwa sana ikiwa utaweza kugundua nini mwenzako anakosa katika maisha yake ya kihisia na kuweza kumpatia kwa ukamilifu.

Wekeza kumbukumbu njema kwa mwenzako. Wekeza raha na furaha katika maisha ya mwenzako. Kumbukumbu njema ambazo unawekeza si tu zitamfanya akukumbuke muda mwingi ila pia hata ikatokea akadanganywa na mtu ila kumbukumbu hizi daima zitamfanya ahisi kupoteza kitu cha thamani katika maisha yake.

Kwa namna hiyo, hata ukitaka kufanya jitihada za kurudiana naye zoezi linakuwa jepesi kwa sababu ya namna unavyoishi katika fikra zake.

Ila shida ipo kama ukiwekeza kero na maudhi. Mwenzako akiwa anakufikiria katika namna hii, ajihisi hata hatia akijiwa na fikra za kutaka kukusaliti kwa sababu atakuwa anajifariji kuwa anakusaliti kwa sababu ya kutafuta amani na raha kitu anachokosa katika maisha yako.

Ili mwenzako akujali na kukupa thamani halisi katika maisha yako, hakikisha unawekeza amani, raha na furaha katika maisha yake. Bila kufanya hivi daima mwenzako hawezi kujivunia kuwa na wewe.

Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya uhusiano, utulivu wa akili na hisia (psychoanalyst).

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU