VIONGOZI WA MATAWI WATAKA YANGA IJITOE KAGAME

VIONGOZI WA MATAWI WATAKA YANGA IJITOE KAGAME

6207
0
KUSHIRIKI

NA SALMA MPELI


VIONGOZI wa matawi ya Yanga wameishauri Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo kuiondoa timu kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame), inayotarajiwa kuanza hivi karibuni, ili wachezaji wapate muda wa kupumzika.

Kauli hiyo ilitolewa juzi, baada ya viongozi hao kukutana katika kikao cha pamoja kilichofanyika makao makuu ya klabu hiyo, yaliyopo Mtaa wa Twiga na Jangwani, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na BINGWA, Mwenyekiti wa tawi la Ubungo Terminal, Stephen Mwakilema, alisema kikao hicho kilijadili mambo mengi, ikiwamo suala la kuutaka uongozi kuiondoa timu kwenye michuano ya Kagame.

“Agenda kuu ya kikao chetu ilikuwa ni kuelekea kwenye mkutano mkuu wa wanachama, lakini pia tulijadili mustakabali wa timu baada ya kutolewa katika mashindano ya SportPesa Super Cup.

“Tumependekeza kama itawezekana timu ijitoe kushiriki Kagame, kwa sababu wachezaji wanakosa muda wa kupumzika.

“Pia tumeitaka kamati ya mashindano kuangalia hilo ili kukipa kikosi nafasi ya kujiandaa na hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, kwa sababu Kagame imekuja nje ya kalenda ya klabu,” alisema.

Hata hivyo, BINGWA lilimtatafuta Mwenyekiti wa Matawi, Bakili Makele na kuzungumzia suala hilo, ambapo alikiri akisema ni kweli katika mambo yaliyojadiliwa suala hilo lilikuwepo.

Aidha, alieleza kuwa, viongozi wa matawi waliokutana katika kikao hicho walikubaliana kuushauri uongozi kujitoa kwenye Kagame ili kuipa timu muda wa kujipanga.

“Tumekuwa tikipata aibu tu, tumemaliza Ligi Kuu nafasi ya tatu, si mbaya, lakini tumetolewa mapema SportPesa Super Cup na kumekuwa na kelele kila siku Yanga haina fedha na timu ni mbovu.

“Kwa kuliona hilo, tumeona ni bora kuipumzisha timu kwa sasa ili tujipange vizuri na kuangalia mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, yaliyo mbele yetu,” alisema Makele.

Aidha, aliongeza kuwa, kikao hicho pia kililenga zaidi kuhusu mkutano mkuu na wamekubaliana kuwahamasisha wanachama kujitokeza kwa wingi ili waingie kwenye mabadiliko.

Hata hivyo, Bakili alieleza kuwa, kwa sasa ni lazima wakubaliane kuingia kwenye mabadiliko ya uendeshaji wa klabu, hivyo wanachama walipie kadi zao ili wapate fursa ya kuingia kwenye mkutano mkuu na kutoa maoni yao.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU