YANGA MBEZI CENTER: MUZIKI WA LWANDAMINA SIMBA HAWAUWEZI

YANGA MBEZI CENTER: MUZIKI WA LWANDAMINA SIMBA HAWAUWEZI

2006
0
KUSHIRIKI

NA MARTIN MAZUGWA

KARIBUNI wasomaji katika safu hii ambayo huwa inawajia kila Jumamosi ikilenga kupata hili na lile kutoka katika matawi ya klabu za soka nchini.

Leo BINGWA limetembelea tawi la Yanga la Mbezi, jijini Dar es Salaam linalofahamika kwa jina la Mbezi Center, ambapo pamoja na mambo mengine limetamba kikosi chao kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo na kutamba kwenye michuano ya kimataifa mwakani.

Akizungumza na BINGWA, Mwenyekiti wa tawi hilo, Abdallah Mohamed, alisema tawi lao lina wanachama 100 ambapo kati yao 80 wakiwa na kadi na wengine 20 wako mbioni kukabidhiwa kadi za uanachama mara baada ya kukamilisha taratibu zote.

Mwenyekiti huyo alisema kwa uwezo walioonyesha katika mchezo dhidi ya JKT Ruvu, hakuna timu ambayo itaweza kuwazuia kubeba taji kwa mara ya tatu mfululizo licha ya kuwa nyuma kwa alama mbili nyuma ya watani wao.

Alisema kuwa si mara ya kwanza kwa watani wao kuongoza ligi kisha kujikwaa kwani hata msimu uliopita waliongoza lakini wakashindwa kuchukua taji hilo ambalo hawajalibeba kwa zaidi ya misimu minne sasa.

Mohamed alisema wao kama Tawi la Mbezi Center wanakiamini sana kikosi chao ambacho mzunguko wa kwanza licha ya kuwa katika hali isiyoridhisha, lakini kilijitahidi kupigana kuhakikisha hakiachwi mbali katika mbio za ubingwa.

Alisema kuwa ligi bado mbichi ndio kwanza mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili wanaamini kikosi chao hakuna wa kuwazuia kama ilivyokuwa kwa msimu uliopita na kuwaacha watani wao katika nafasi ya tatu.

Kwa upande wa benchi la ufundi wamefurahishwa na uongozi kulifanyia marekebisho kwa kumkabidhi George Lwandamina ambaye ameonyesha uwezo wa hali ya juu katika mchezo wake wa kwanza licha ya kuwa mgeni wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ameonyesha kuwa na kitu cha ziada hasa jinsi alivyo na uwezo wa kuangalia mchezo kwa jicho la tatu, kwani mabadiliko aliyoyafanya katika mchezo dhidi ya JKT Ruvu kwa kumtoa mshambuliaji na kumwingiza kiungo kiliwaacha mashabiki wengi midomo wazi.

Anapaswa kupewa muda naamini atakuwa na msaada mkubwa siku za baadaye, kutokana na uwezo wake wa kuzoea mazingira haraka.

Mohamed alisema kuwa mipango ambayo wamejiwekea msimu huu ni pamoja na kuhakikisha mtani wao hachezi mechi nje ya uwanja, watahakikisha wanaziba mianya yote ya udanganyifu pindi watakapokuwa wanashuka uwanjani dhidi ya mnyama.

Alisema mbali na rushwa watahakikisha wanakuwa makini na vitendo vya kishirikina kama vilivyotokea katika mzunguko wa kwanza walipokamata vitu vinavyodhaniwa kuwa vya kishishirikina vilivyoletwa na wapinzani wao.

Pia mwenyekiti huyo aliwataka wanachama wa klabu ya Yanga kuwa kitu kimoja ili kuhakikisha wanachukua ubingwa malengo ambayo wamejiwekea msimu huu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU