NA HUSSEIN OMAR
KOCHA wa Yanga, George Lwandamina, juzi aliwachezesha wachezaji wake wote katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Singida United uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hali iliyopokewa tofauti na mashabiki wa timu hiyo.
Kitendo hicho kilionekana kuwashangaza baadhi ya mashabiki wa Yanga ambao walitamani kuona kikosi cha kwanza kikipikwa zaidi kupitia mchezo huo.
Hali hiyo ilikuwa ni tofauti na alivyofanya Kocha wa Singida United, Hans van der Pluijm ambaye hakufanya mabadiliko makubwa katika kikosi cha kwanza.
Kikosi alichoanza nacho, alikipa muda wa kutosha na kufanya mabadiliko ya wachezaji wachache, huku Lwandamina akiwabadili wote.
Japo wapo waliompinga Lwandamina, kilichoonekana ni kwamba kocha huyo alitaka kuwaonyesha mashabiki wao aina ya wachezaji waliosajiliwa na viongozi wao.
Katika mchezo huo, kuna wachezaji wapya ambao walionyesha kiwango cha chini waliosajiliwa msimu huu ili kuiwezesha timu hiyo kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na kutikisa kwenye michuano ya kimataifa mwakani.
Kitendo cha Lwandamina kuwachezesha wachezaji wake wote, hasa wale wapya, kwa kiasi fulani kimewavua nguo waliosimamia usajili wa timu hiyo.
Hilo linatokana na viwango vya baadhi ya wachezaji kama yule aliyecheza beki namba tatu kutoka Nigeria, Henry Okoh na wengineo wapya.
Mwisho wa siku, Lwandamina hakutaka ‘shobo’ aliona ni vema akawaanika wachezaji wake wote, hasa wapya, ili mashabiki wawaone na hatimaye kuwapima wenyewe iwapo wanaweza kuwawezesha kutetea ubingwa wao au la.
Kwa kifupi, tunaweza kusema kuwa Lwandamina ni mjanja sana aisee, ni kama vile alitaka ‘kuwashtaki’ viongozi wa Kamati ya Usajili mbele ya mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kutokana na kile alichokifanya Uwanja wa Taifa Jumamosi.