MICHAEL MAURUS NA MARIAM SHABANI (TUDARCO)
“YAANI (Haruna) Niyonzima katufanyia vile kweli, kava jezi nyekundu hivi hivi…dah! Inauma sana kwa kweli.”
Hayo ni maneno ya mmoja wa wapenzi wa Yanga aliyeyatoa mara baada ya kumshuhudia Niyonzima akitambulishwa na viongozi wa Simba jana kama mmoja wa wachezaji wao wapya waliowasajilio kwa ajili ya msimu mpya unaotarajiwa kuzinduliwa Agosti 23, mwaka huu kwa mchezo wa Ngao ya Jamii.
Hilo limekwua ikiwa ni baada ya wiki kadhaa kuelezwa kuwa kiungo huyo aliyekipiga Yanga kwa takribani misimu sita, amesajiliwa na Simba.
Hata hivyo, Simba walichelewa kumtambulisha au kutamka hadharani kuwa wamemalizana na Niyonzima kwa kuwa bado alikuwa na mkataba na Yanga ambao ulifikia tamati Julai 23, mwaka huu.
Na hata baada ya mkataba wake na Yanga kumalizika, bado Niyonzima hakuweza kuonekana hadharani akiwa katika sura ya ‘Mnyama’ hadi ilipokuwa hivyo jana ambapo asubuhi alihudhuria mazoezi kwenye Uwanja wa Boko Veterans, Dar es Salaam na mchana kutambulishwa makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Mtaa wa Msimbazi.
Hatimaye ni wazi kwa sasa mashabiki, wanachama na viongozi wa Simba watakuwa na maneno matatu tu ya kuwaambia wale waliokuwa hawaamini kama kiungo huyo amesaini Msimbazi kwa kuwaambia ‘Njooni Mjionee Wenyewe’.
Maneno hayo hayatamhusu Niyonzima pekee, bali wapinzani wa Simba pamoja na mashabiki wa klabu hiyo, leo watapata fursa ya kuwaona wachezaji wao wengine wapya, akiwapo aliyekuwa ‘Mfalme wa Msimbazi’, Emmanuel Okwi, Mghana Nicholas Gyan, Jamal Mwambeleko, Aishi Manula, Shomari Kapombe na Said Mohammed ‘Nduda’.
Wengine ni Salim Mbonde, Ally Shomari, Erasto Nyoni, Emmanuel Mseja, John Bocco na wengineo ambao wataungana na wale waliopo kikosini kuivaa Rayon Sports ya Rwanda katika mchezo wa kirafiki ambao ni sehemu ya tamasha la klabu hiyo la Simba Day kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo.
Ukiachana na wachezaji, ni wazi mashabiki wa Simba leo watakuwa na shauku ya kuona ubora wa kikosi chao, hasa baada ya Yanga kuchezeshwa mchakamchaka na Singida United katika mchezo wao wa kirafiki Jumamosi iliyopita kwenye uwanja huo.
Mashabiki wa Simba watakapokuwa uwanjani leo, watatamani watani wao wa jadi, Yanga, nao wawepo ili kujionea wenyewe ‘muziki’ wa kikosi chao, lakini pia vitu adimu vitakavyoonyeshwa na wachezaji wao, hasa Niyonzima, Okwi, Bocco na Gyan.
Tamasha la Simba Day ambalo mwaka huu linafanyika kwa mara ya 10 tangu lilipoanza ramsi mwaka 2008 chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali, kama ilivyo ada, leo litaambatana na matukio kadha wa kadha, ikiwamo kutambulisha wachezaji wao wapya, lakini pia kukumbuka michango ya baadhi ya wachezaji na viongozi wao.
Pia, jezi mpya za timu hiyo zitatambulishwa ambapo tukio hilo likisindikizwa na burudani kutoka kwa wasanii wa hapa nchini, akiwamo Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, Ommy Dimpoz, Tunda Man anayedaiwa kutunga wimbo maalum kwa ajili ya tukio hilo na wengineo.
Kama ilivyo utamaduni wa siku hiyo, wapenzi wa Simba, wakiwamo viongozi wa serikali na wafanyabiashara maarufu, wanatarajiwa kufurika Uwanja wa Taifa leo kushuhudia ‘silaha’ zao za msimu wa 2017/18.
Msimu uliopita, Simba ilishika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ikifanikiwa kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la FA Tanzania.