NA MARTIN MAZUGWA
ETI kapiga mkwara! Kiungo kipenzi cha mashabiki wa klabu ya Simba, Emmanuel Okwi, amesema mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara klabu ya Yanga, hawatatoka salama katika mchezo wa Ngao ya Hisani utakaopigwa Agosti 23 katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Okwi alisema hayo mara baada ya kumalizika mchezo dhidi ya Rayon Sports, ulioisha kwa Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Mohamed Ibrahim ‘Mo’.
Mshambuliaji huyo anayetambulika kama ‘mfanyabiashara’ kutokana na kuuzwa mara mbili na klabu ya Simba kwa klabu za Etoile Du Sahel, Tunisia na SønderjyskE ya Denmark, alijiunga na Wekundu hao msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili, akitokea katika klabu ya SC Villa ya nchini Uganda alipokwenda kulinda kiwango chake.
Akizungumza na BINGWA, Okwi alisema kwa maandalizi waliyoyafanya hakuna timu itakayowazuia hivi sasa na wanaanza na watani wao wa jadi katika mchezo wa Ngao ya Hisani, hivyo kuwataka mahasimu wao kujiandaa kisaikolojia.
“Maandalizi yetu yameenda vizuri wachezaji wote wana ari ya juu, sidhani kama kuna timu itatoka salama na tunaanza kampeni yetu na Yanga.
“Simba ya sasa imesheheni, sitaki kuwa mzungumzaji sana naamini mtayaona hiyo Agosti 23, kwani hawatatoka salama,” alisema Okwi.
Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wa timu hiyo walitamba kuwa huenda kikosi hiki kinaweza kutoa kipigo kikubwa tena kwa Yanga kama kile cha Mei 6, 2012.
Yanga ilikubali kipigo hicho kutoka kwa vijana wa Simba wakati huo kikosi kikiundwa na Mzambia Felix Sunzu, Patrick Mutesa Mafisango, Haruna Moshi ‘Boban’, Kelvin Yondani, Uhuru Selemani, Nassoro Said ‘Chollo’, Mwinyi Kazimoto, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Juma Kaseja na Mganda Emmanuel Okwi, huku kocha akiwa Mserbia Milovan Cirkovic.
Okwi alifunga mabao mawili, Mafisango (penalti) mbili, Kaseja (penalti) moja. Penalti tatu zilitolewa katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Hashim Abdallah wa Dar es Salaam na kuweka historia ambayo haijafutwa hadi leo.
Kikosi cha Simba kwa sasa kimebakiwa na wachezaji watatu ambao walishiriki kuipa Yanga kipigo hicho cha mbwa mwizi cha mabao 5-0, ambao ni Okwi, Jonas Mkude na Mwinyi Kazimoto.
Mmoja wa mashabiki hao aliyejulikana kwa jina la Kisugu alisema anakiona kipigo kingine cha aibu kwa Yanga.
“Niseme nini mimi Kisugu, Niyonzima na Okwi washasema kila kitu, sidhani kama kuna maneno maneno tena, nakiona kipigo kingine kikubwa kwa Yanga,” alisema shabiki huyo.