LONDON, England
KWA lugha nyingine unaweza kusema ni kama bundi kaanza kulia, baada ya tatizo la kukumbwa na majeraha linaloonekana kuanza kumtesa mapema kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, hata kabla msimu haujaanza.
Kwa mujibu wa gazeti la Metro, straika Alexis Sanchez, atazikosa mechi mbili za kwanza kutokana na matatizo ya tumbo na huku mastaa wengine, Aaron Ramsey na Mesut Ozil, nao kuendelea kuwa shakani kutokana na matatizo ya kifundo cha mguu na enka, ambayo yaliwafanya kuikosa mechi ya Ngao ya Jamii iliyopigwa Jumapili iliyopita dhidi ya Chelsea.
Mbali na nyota hao, pia staa mwingine ni Shkodran Mustafi ambaye naye hayupo fiti kiafya na hawezi kuwamo kwenye kikosi cha kwanza na hadi sasa, amepewa likizo ndefu baada ya kushiriki katika michuano ya mabara na huku mwenzake Per Mertesacker alilazimika kupumzishwa wakati wa mchezo huo wa Jumapili uliopigwa kwenye Uwanja wa Wembley, baada ya kugongwa kwa kiwiko na staa wa Chelsea, Gary Cahill.
Nyota wengine ni Gabriel na Santi Cazorla ambao watakosekana kwa muda mrefu na huku kukiwa hakuna tarehe maalumu ya kurejea uwanjani, Jack Wilshere na Francis Coquelin ambaye aliumia goti wakati wa mchezo wa Kombe la Emirates ambao waliibuka na ushindi dhidi ya Benfica.
Kukosekana kwa mastaa wote hao inaonekana huenda ukawa mwanzo mbaya kwa Wenger ambaye kesho usiku ataikabili Leicester City kwenye Uwanja wa Emirates.